Sh796 milioni kuwanufaisha wananchi kituo cha afya Chunya

Chunya. Serikali imetoa zaidi ya Sh 796 milioni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mbugani, Kata ya Mbugani, Wilaya ya Chunya ili kuwapunguzia adha wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

Mradi huo utahudumia wananchi zaidi ya 15,000 ambao awali walikuwa wakitegemea  huduma za afya kwenye zahanati ya Chalangwa na Hospitali ya Wilaya ya Chunya.

Akizungumza na Mwananchi Digital Januari 12, 2026, Diwani wa Kata ya Mbugani, Bosco Mwanginde amesema lengo la uwepo wa mradi huo ni kupunguza adha ya wananchi hususani kina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya mikakati ya kuboresha huduma muhimu kwa jamii katika kutekeleza sera ya afya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Kwa miaka mingi kata hii ilikuwa haina zahanati wala kituo cha afya, lakini katika kipindi  cha miaka mitano tuliweza kujenga  mbili kwenye Kijiji cha Mbugani na Mlima Njiwa jambo ambalo lilichangia  muingiliano  mkubwa wa wananchi kufika kupata huduma,” amesema.

“Kwa sasa tayari Serikali imetupa  Sh796 milioni, ambazo zitaingizwa kwa ajili ya kuanza mchakato wa manunuzi jambo ambalo litarejesha kicheko kwa wananchi kupata huduma jirani na maeneo waishio,”amesema.

Mwanginde ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chunya kwa vipindi vya miaka 10, amewaomba wananchi kushiriki nguvu kazi katika kutekeleza mradi huo.

“Niwaombe wananchi mbali ya Serikali kutoa fedha hizo pia jitokezeni kushiriki nguvu kazi sambamba na kutoa ushirikiano kwa watendaji wakipita kuchangisha fedha lengo ni kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa wakati,”amesema.

Wakati huohuo, diwani huyo amehamasisha vijana kutumia fursa ya kujiunga na mafunzo ya uanagenzi katika muhula mpya ambao Serikali imetangaza ili kujiongezea ujuzi.

“Katika Kata yangu Serikali imejenga Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), lakini mwamko wa vijana ni mdogo kufuatia idadi kubwa kukimbilia kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu na kupelekea uhana wa wanafunzi kukimbilia fursa hiyo,” amesema.

Mwanginde ameishauri Serikali kupitia uwekezaji huo kuona namna bora ya kuongeza mitaala inayo endana na shughuli za uchimbaji wa madini ili kuvutia wengi zaidi kupata ujuzi.

“Unajua asilimia kubwa licha ya kuhakikisha tuna hamasisha vijana kujiunga Veta, bado ni wazito wanaona kukaa darasani wanapoteza muda wa kuingiza fedha za papo hapo kwenye machimbo ya madini ya dhahabu,” amesema.

Subira Mwakyusa Mkazi wa Kijiji cha Mbugani, amepongeza Serikali kuja na mkakati wa ujenzi wa Kituo cha Afya kuwa mkombozi na kuokoa muda wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali, lakini pia Diwani wetu mpambanaji kwa kuona umuhimu wa kuomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao mbali na kutoa huduma hutachoche shughuli za kiuchumi na ajira kwa vijana, ” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya, Tamim Kambona amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miradi ya huduma za afya hususani upatikanaji wa vifaa tiba.

Amesema, pia halmashauri itaendelea kuunga  mkono jitihada za Serikali kwa kutenga mapato ya ndani asilimia 10 ,kwa kila mwaka  kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo katika  sekta ya afya, elimu, maji na barabara kwa kununua mtambo wa kuchonga.