Shinikizo kuachiwa wafungwa wa kisiasa 751 Venezuela latua kwa Papa

Vatcan. Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, María Corina Machado, amezungumza na Papa Leo wa Kumi na Nne (XIV) siku ya Vatican na kumuomba kuongeza shinikizo kuachiwa wafungwa wa kiasiasa takribani 751 wanaoshikiliwa na serikali ya Venezuela.

Machado amewaambia waandishi wa habari jana Jumatatu Januari 12, 2026 kuwa amemwomba Papa Leo aingilie kati ili kusaidia kuachiwa kwa mamia ya wafungwa wa kisiasa ambao bado wanazuiwa katika nchi hiyo iliyopo Amerika Kusini.

Papa Leo amesema kuwa anafuatilia kwa ukaribu yanayoendelea nchini Venezuela, na akatoa wito wa kulindwa kwa haki za binadamu na haki za kiraia katika nchi hiyo.

Nchini Venezuela, familia za watu waliokamatwa au kutoweka bado zilikuwa zikisubiri nje ya gereza ambako wapendwa wao wanashikiliwa.

Hadi kufikia Jumatatu alasiri, wafungwa wa kisiasa 49 pekee kati ya zaidi ya 800 walikuwa wameachiliwa huru, licha ya ahadi ya serikali kuachia “idadi kubwa” ya wafungwa hao.

Upinzani wa Venezuela kwa muda mrefu umekuwa na matumaini ya kumwondoa Rais Nicolás Maduro na kumweka madarakani mmoja wao ili kurejesha demokrasia nchini humo.

Hata hivyo, baada ya majeshi ya Marekani kumkamata Maduro na kumpeleka New York kukabiliwa na mashtaka ya biashara ya dawa za kulevya, Rais Trump alimruhusu naibu wake, Delcy Rodríguez, kuchukua uongozi wa nchi hiyo.