Simanjiro yafanya mageuzi ya kilimo

Simanjiro. Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, imejipanga kuhakikisha inafanya mageuzi makubwa katika mazao ya kilimo na mifugo ili wakazi wa eneo hilo wapate tija zaidi kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala ameeleza hayo Januari 13, 2026 kwenye kongamano la kilimo linalofanyika mji mdogo wa Orkesumet

Lulandala amesema Simanjiro ina maeneo makubwa ya kilimo yenye rutuba ikiwemo ya umwagiliaji ila bado hayajatumika ipasavyo katika kulima.
“Simanjiro imetenga kiasi cha hekta 17,000 kwa ajili ya kilimo ila hadi sasa watu wanatumia hekta 630 pekee kwa kulima, tunawakaribisha wakilima waje Simanjiro kwani tumejipanga kisawasawa,” amesema DC Lulandala.

Mkuu huyo wa wilaya ametaja baadhi ya mazao yanayostawi kwenye eneo hilo ni mahindi, maharage, vitunguu, mpunga na ufuta.
Hata hivyo, amewaagiza maofisa ugani kuhakikisha wanahamia mashambani kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima na kutobakia maofisini kwao.
Maofisa ugani ofisi zenu ziwe mashambani badala ya ofisini kwani waajiri wetu wanapatikana mashambani hivyo tusikae maofisini kwetu,” amesema Lulandala.

Mmoja kati ya wakulima katika wilaya hiyo, Ibrahim Abdallah ameeleza kwamba kongamano hilo limekuwa na manufaa kwa wakulima kwani watakuwa na uhakika wa kupata pembejeo za kilimo kwa wakati tofauti na awali.
Abdallah amesema awali walikutana na changamoto ya  kutopata mbegu zenye ubora, hivyo kupata wakati mgumu kuvuna mazao ya maana ila kupitia kongamano hilo la mazao ya kilimo mbegu nyingi zenye ubora zimewafikia.

Bwana shamba mauzo wa kampuni ya mbegu ya Seedco, Peter Timotheo ameeleza kwamba wanawajali wakulima wa Simanjiro kwa kuwapatia mbegu bora kwani mavuno bora huanza na mbegu bora.

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara Fakii Lulandala (katikati) akikagua baadhi ya mabanda kwenye kongamano la kilimo linaloendelea mji mdogo wa Orkesumet, kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Gracian Max Makota. Picha na Joseph Lyimo

Timotheo amewaasa wakulima hao kuhakikisha wanachangamkia fursa ya kuwepo kwa mbegu  bora na kuzichukua ili wapate mavuno bora.