Dar es Salaam. Jamhuri imepanga leo Jumanne, Januari 13, 2026 kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo, wafanyabiashara sita wanaokabiliwa na kesi ya kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam na kujipatia zaidi ya Sh10bilioni zilizotokana na shehena ya mafuta.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi kukamilika.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Joseph Matage; Grace Matage ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya RHG General Traders Ltd na pia ni wakala wa forodha; Jamaal Saad; Mubinkhan Dalwai; Stanley Tibihenda na Edward Omeno ambao wote ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba katika Mahakama ya 5195 ya mwaka 2025 katika Hakimu Mkazi Kisutu.
Kesi hiyo ina jumla ya mashtaka 13 yakiwamo ya kula njama, kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam na kujipatia Sh10 bilioni zilizotokana na shehena ya mafuta.
Washtakiwa baada ya kusomewa maelezo na vielelezo hivyo, kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusubiri kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.
Tarehe hiyo ilipangwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, anayesikiliza kesi hiyo, baada ya upande wa jamhuri kuieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi umeshakamilika na tayari wameshasajili nyaraka muhimu Mahakama Kuu.
Hata hivyo, washtakiwa wote wapo rumande kutoka na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Februari 28, 2025 na kusomewa mashtaka yao.
Kati ya mashtaka hayo 13; matano ni ya kughushi nyaraka, matano ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam, moja la kuongoza genge la uhalifu, jingine ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kutakatisha fedha.
Katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Juni mosi na Novemba 30, 2024 katika Jiji la Dar es Saalm na maeneo mengine, washtakiwa kwa nia ovu, waliandaa genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh6 bilioni.
Katika shtaka moja wapo la kughushi nyaraka, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Julai mosi na Agost 12, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu, walioghushi nyaraka ya uongo iitwayo Delivery Order yenye kumbukumbu namba APU 04638 ya Agosti 12, 2024 kwa kuonyesha kuwa ni halali na imetolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd, kupitia wakala wa meli Maersk Group, wakati wakijua kuwa nyaraka hizo ni za uongo.
Katika shtaka moja wapo la kuwasilisha nyaraka ya uongo, washtakiwa wanadaiwa Agosti 12, 2024 kwa njia ya udanganyifu waliwasilisha nyaraka hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuonesha kuwa ni halali na imetolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd kupitia wakala meli Maersk Group, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Vilevile katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Juni mosi na Novemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu walijipatia kilo 6,367,262 za mafuta ya kupikia aina Camar zenye thamani ya Sh10bilioni mali ya kampuni ya AAstar Trading PTE Ltd kwa kudanganya kwamba bili halisi ya shehena ya mafuta ilitolewa na Kampuni ya Nyota Tanzania Ltd kupitia Maersk Group, wakati wakijua kuwa ni uongo.
