Yanga yailazimisha Pamba irudi sokoni

DILI la kipa Yona Amosi wa Pamba Jiji kutua Yanga lipo hatua za mwisho na jambo hilo limelifanya benchi la ufundi la chini ya kocha Francis Baraza kurudi sokoni haraka kusaka mbadala wa kipa na nahodha huyo wa kikosi hicho  jijini Mwanza.

Kipa huyo aliyeshika namba mbili ya makipa wazawa waliofanya vizuri msimu uliopita akiwa na clean sheet 11, nyuma ya Patrick Munthari wa Mashujaa, aliyekuwa na 14 inadaiwa amemalizana na Yanga, huku Simba nayo ikimpigia hesabu akiwa amebakiza miezi sita kuitumikia Pamba Jiji.

Wakati ikiripotiwa hivyo Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na Baraza kufahamu usajili unaendeleaje ndani ya kikosi hicho, ndipo alipoweka wazi kuwa bado hawajafanikiwa kusajili lakini mpango ni kuongeza beki wa kati na kipa.

“Hadi sasa hivi tunavyozungumza bado sijaanza kusajili, ila kama ni kuongeza itabidi niongeze beki wa kati kutokana na kuondoka kwa Abdallah Kheri ‘Sebo’, bila hivyo pia mchakato wa beki ya kati ulikuwa unafanyika lakini pia na eneo la kipa,” amesema kocha huyo Mkenya na kuongeza;

YON 01

“Sijataja kuwa Yona anaondoka ila kuna utaratibu wa kuongeza wachezaji katika sehemu nilizotaja kuhusu kipa wetu namba moja kuondoka sina taarifa hizo nasikia kama unavyosikia wewe.”

Baraza amesema tetesi zipo, hivyo hawezi kuongelea mchezaji ambaye yupo naye kwenye uwanja wa mazoezini kama biashara itafanyika basi atakuwa kwenye nafasi ya kuzungumza.

“Sasa ni dirisha la usajili mengi yanazungumzwa hivyo kuhusu Yona kuondoka mengi yanasemwa, lakini mimi kama kocha sina taarifa rasmi ila mchakato wa kuongeza mchezaji kwenye nafasi yake unaendelea,” amesema Baraza aliyewahi kuzinoa timu kadhaa hapa nchini na kule kwao Kenya ikiwamo Tusker.

YON 02

“Tunatakiwa kuongeza nguvu kikosini kwa kuzingatia mahitaji uongozi umepata ripoti na unafanya kazi kwa sasa timu inaendelea na maandalizi tayari kwa kurudi kwenye ushindani,” alisisitiza kocha huyo aliyeiongoza Pamba Jiji katika Ligi ya msimu huu kucheza mechi tisa na kushinda nne, kutoka sare nne na kupoteza moja, ikivuna pointi 16 ikilingana na Yanga.

Pamba ipo nafasi ya tatu nyuma ya Yanga kwa tofauti na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, kwani yenyewe imefunga 11 na kufungwa sita, ilihali Yanga imekwamisha 12 na kufungwa moja kupitia mechi sita ilizocheza ikiwa nyuma ya JKT Tanzania yenye pointi 17.