Yule Messi wa Simba yupo tayari kuliamsha

KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Simba, Azam FC na TP Mazembe, Ramadhan Singano ‘Messi’ amezungumzia kilichokuwa nyuma ya ukimya wake na utayari wa kurejea tena uwanjani ili kuweza kuendeleza kipaji chake.

Singano amesema alipata changamoto ya kimkataba akiwa na TP Mazembe aliyokuwa amejiunga nayo 2019/20, baada ya mwaka jana kumalizika anaona anaweza akaendelea na mambo yake.

“Nilijiunga na TP Mazembe kwa mkataba wa miaka mitano ilikuwa 2019/20 yapo mambo hayakwenda sawa baada ya wao kunitoa kwa mkopo kwenda Nkana ya Zambia mwaka 2021,” amesema Singano na kuongeza:

“Sipendi kabisa kulizungumzia jambo hilo, ila nadhani hadi hapo watu wataelewa kwa nini nilikaa kimya.”

Alipoulizwa anajutia kujiunga na timu hiyo? Alijibu:”Hapana kwani nilipata nafasi ya kujifunza ushindani mkubwa… ushindani wa namba ndio sababu ya kupelekwa Nkana. Kilichosumbua ilikuwa ni kushindwa kutimiza baadhi ya vipengele vilivyokuwa katika mkataba.”

Vipi kuhusu kurejea kucheza tena? Amesema pamoja na ukimya bado alikuwa anaendelea kufanya mazoezi kama kawaida akiwa fiti na timu itakayotaka kufanya naye kazi yupo tayari.

“Kama ikitokea timu itanihitaji nipo tayari, ingawa pia nina kituo ninachofundisha watoto ninaotamani wazifikie ndoto zao,” amesema Singano aliyefahamika zaidi kwa jina la Messi kipindi akiibuka katika soka la vijana kutokana na uwezo wa kupiga chenga kwa mguu wa kushoto kama nyota wa kimataifa wa Argentina aliyekuwa akimpenda na kumfuatilia.