Ado Shaibu na Devotha Minja wapewa kamati nyeti, kati ya 17 za Bunge  

Dodoma. Bunge la 13 limeunda jumla ya kamati 17 huku kamati nyeti zikikabidhiwa kwa wabunge wa upinzani wa Chaumma na ACT Wazalendo.

Majina ya vigogo yamechomoza kwenye kamati hizo huku baadhi ya wabunge wakongwe wakirejea katika uongozi wa kamati walizoongoza Bunge la 12.

Kamati zilizopewa wapinzani ni Hesabu za Serikali (PAC) ambayo amekabidhiwa Devotha Minja na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo itaongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu.

Hii ni mara ya kwanza wapinzani kutoka vyama viwili tofauti wanaongoza kamati hizo ambazo kwa kipindi kirefu zilikuwa chini ya wabunge kutoka Chadema.

Katika taarifa iliyotolewa leo na  Bunge, Devotha Minja atasaidiana Khalifan Aeshi ambaye amechaguliwa kuwa makamu huku Kamati ya (LAAC) Makamu wake ni Abdallah Chikota.

Katika Bunge la 12 Kamati ya PAC iliongozwa na Naghenjwa Kaboyoka wakati Kamati ya LAAC Mwenyekiti wake alikuwa Halima Mdee wote wakitokea Chadema, licha ya kuingia kwenye msukosuko wa kutimuliwa na chama chao.

Minja na Ado Shaibu wamepewa Kamati hizo ambazo zimekuwa na hoja nzito kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo mara nyingi mashirika na halmashauri yametajwa kuwa na mapungufu ya mifumo ya kimanunuzi na kupelekea upotevu mkubwa wa fedha.

Kamati zingine zilizoundwa ni Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo Mwenyekiti wake ni Anne Kilango Malecela na Makamu wake ni Christina Mndeme, huku Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Mwenyekiti ni Masanja Kadogosa na Makamu wake Dougras Masaburi.

Kamati ya Sheria Ndogo itaongozwa na Cecilia Pareso na Makamu wake ni Yahya Zuberi lakini Kamati ya Utawala,Katiba na Sheria wamepewa wabobezi wa sheria ambapo Mwenyekiti ni Dk Damas Ndumbaro na Makamu wake ni Edwin Swale.

Mashimba Ndaki ameendelea kuongoza Kamati ya Bajeti na Makamu wake ni Ally Hassan King. Naibu waziri wa nishati wa zamani Subira Mgalu amechaguliwa Kamati ya Nishati na Madini akisaidiwa na Simoni Lusengekile.

Mbunge Mpanda, Seleman Kakoso amerudi kwenye nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu akisaidiana na Abubakari Asenga huku Kamati ya Afya na Masuala ya Ukimwi wamechaguliwa Dk Johannes Lukumay kuwa Mwenyekiti na Zeyana Abdallah Hamid ndiye Makamu.

Mbunge mwingine aliyerudia nafasi yake ni Timotheo Mzava ambaye ameendelea kuwa Mwenyekiti Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Makamu wake ni Mary Masanja na Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo Husna Sekiboko atasaidiana na Cornel Magembe.

Kamati zingine ni Maji na Mazingira iliyorudi tena kwa Jackson Kiswaga nafasi ya Makamu ikienda kwa Profesa Pius Yanda na Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii itaongozwa na Hawa Machafu Makamu ni Regina Malima.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la 12, Nagma Giga safari hii amepewa kuongoza Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Makamu ni Mbunge wa Dodoma, Paschal Chinyele. Kamati ya Viwanda, Biashara na Kilimo ameendelea Deodatus Mwanyika na Makamu wake amerudi Mariam Ditopile.

Kwenye Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) amechaguliwa Florence Kyombo atasaidiana na Jafari Chege.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ndogo, Cecilia Pareso ametaja mkakati anaoingia nao ni kuhakikisha sheria ndogo hazikinzani na sheria mama.

Pareso amesema kwa sasa ni mapema zaidi kuzungumzia mikakati mikubwa kwani anahitaji kukaa na wajumbe wake lakini anachotamani kuwepo na sheria kinzani.

Mbunge wa Jimbo la Handeni, Charles Sungura (Kamati ya LAAC) amesema ana imani kubwa na uongozi wa kamati hiyo kutokana na mchanganyiko wa wabunge wa chama tawala na upinzani, hivyo ni kamati itakayofanya vizuri na Watanzania watapata manufaa yake.

Sungura amesema umoja ndio silaha pekee wanayojivunia kwenda kujitofautisha na kamati zingine kwani kazi yao ni kwenda kusimamia sheria, hivyo mambo mazuri yanakuja.