Arusha Yageuza Bodaboda Kuwa Fursa Mpya

Na Pamela Mollel,Arusha.

Jiji la Arusha limeanza ukurasa mpya katika sekta ya bodaboda baada ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, kuzindua mradi wa kukopeshana pikipiki sambamba na mkakati wa kurahisisha upatikanaji wa leseni.

 Hatua hiyo inalenga kuwawezesha vijana kiuchumi na kubadili taswira ya bodaboda kutoka kelele za barabarani hadi ajira halali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkude alisema bodaboda si tatizo, bali changamoto kubwa ni mfumo mgumu wa leseni na ukosefu wa usimamizi. 

Alisisitiza kuwa kufuata sheria za usalama barabarani ni wajibu, lakini serikali ina jukumu la kuweka mazingira rafiki kwa vijana wanaojitafutia kipato.

Katika kuwasaidia madereva wengi kuingia rasmi kwenye mfumo, DC Mkude alipendekeza mpango wa kugharamia leseni kwa pamoja, ambapo waendesha bodaboda watachangia nusu ya gharama huku wadau wakilipia nusu iliyobaki. 

Hata hivyo Madereva wametakiwa kujiandikisha ili mpango huo utekelezwe kwa uwazi na ufanisi.

Pia aliagiza Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha kupunguza urasimu katika utoaji wa leseni, akisisitiza kuwa mafunzo ya siku moja yanatosha kwa madereva wanaoendesha kama biashara, badala ya kuwapeleka VETA kwa muda mrefu.

Pamoja na hatua hizo za kuwezesha, Mkude alisema operesheni dhidi ya pikipiki zitakazokiuka sheria zitaendelea, hasa kwa wahuni wanaosababisha fujo mitaani. Alisema dereva bodaboda anayejitambua hawezi kuhatarisha biashara yake kwa vitendo visivyo vya kistaarabu.

Kwa upande wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Jiji la Arusha, mwenyekiti wake Shwahibu Hamisi alisema umoja huo umeanza mradi wa kukopeshana pikipiki kwa kushirikiana na kampuni ya TVS, ambapo pikipiki 20 tayari zimekopeshwa kwa awamu ya kwanza kwa fedha zilizochangwa.

Kwa ujumla, mradi huu unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuwawezesha vijana wa Arusha, kupunguza ajali bara8barani na kuifanya bodaboda kuwa sekta rasmi yenye mustakabali mzuri wa kiuchumi na ajira.