Kyiv. Mamlaka nchini Ukraine zimelazimika kusitisha baadhi ya safari za treni kwenye maeneo kadhaa nchini humo kutokana na uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na barafu.
Barafu hiyo imesababishwa na theluji iliyotokea baada ya mvua kunyesha kwa katika maeneo ya taifa hilo ikiwemo kwenye mji mkuu Kyiv.
Meya wa Jiji la Kyiv, Vitali Klitschko, amesema changamoto hiyo imetokana na baridi kali kuathiri vituo vya umeme, vituo vya kuhifadhia nishati na miundombinu mingine muhimu ndani ya jiji hilo.
Hivyo wakazi wa jiji, hilo wanapaswa kuondoka Kyiv ili kusaidia kupunguza shinikizo kwenye matumizi ya rasilimali muhimu.
“Treni zilizositishiwa safari ni za Ukraine ambazo huendeshwa kwa kutumia dizeli,”amesema Klitschko.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa treni hizo kwa sasa zimelazimika kukaa kwenye kituo cha reli cha mjini Kyiv, huku mabehewa yake yakitumika kutolea huduma za kijamii ikiwemo malazi kwa waathirika wa mapigano yanayoendelea nchini humo.
Wakati hayo yakijiri, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ameishutumu Russia kwa kutumia kimakusudi majira ya baridi kali kulenga vituo vya umeme, vituo vya kuhifadhia nishati na miundombinu mingine muhimu. Amesema mashambulizi katika vituo vya nishati yamesababisha kukatika umeme.
Imeandaliwa na Elidaima Mangela kwa msaada wa mashirika ya habari.