DC Arusha alivyozima mgomo wa wafanyabiashara

Arusha. Mgomo wa wafanyabiashara wa maduka jijini Arusha uliokua umeitishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa wafanyabiashara, Rocken  Adolf umesitishwa kupisha majadiliano yaliyoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude ili kupata suluhu la kudumu la mgogoro huo ambao umekua ukiibuka mara kwa mara.

Wafanyabiashara wenye maduka wanalalamika kushindwa kuendesha biashara zao kwa uhuru na kulingana masharti ya leseni, kutokana na wachuuzi maarufu machinga kupanga bidhaa zao mbele ya maduka yao jambo linalosababisha wateja kushindwa kuingia, hivyo kupata hasara.

Kupitia taarifa aliyoitoa jana Januari 13, 2026 kwa waandishi wa habari, Adolf alitangaza mgomo usio na kikomo wa wafanyabiashara wenye maduka wapatao 14,000 kwa lengo la kushinikiza Serikali kuchukua hatua za haraka ili kunusuru biashara zao.

“Tumekua tukifanya vikao vya mara kwa mara na viongozi wa serikali za mitaa na wilaya lakini ufumbuzi wa changamoto umekua haupewi kipaumbele, tunashindwa kuelewa kwa nini maamuzi hayachukuliwi wakati machinga wametengewa maeneo ya kufanyia biashara kwa uhuru na sio kuzipanga mbele ya maduka yetu,” alisema Adolf.

Leo Jumatano, Januari 14, 2026 Mkude alitembelea mitaa inayolalamikiwa na kuzungumza na machinga pamoja na wafanyabiashara wenye maduka kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.

Mkude amewaagiza machinga kufanya shughuli zao kwenye maeneo yaliyotengwa ambayo ni masoko ya Machame, Ulezi, Kilombelo, Samunge na Majengo ya Juu na kuacha kupanga bidhaa zao mbele ya maduka ya wafanyabiashara wanaolalamika kukosa wateja kwa sababu yao.

Mkuu wa wilaya ya Arusha,Joseph Mkude akizungumza na wafanyabiashara wenye maduka waliopanga bidhaa zao kwenye njia za watembea kwa miguu kuziondoa mara moja katika mtaa Sabena jijini Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu

“Nimejionea mwenyewe na nitafika kwenye hayo masoko yaliyotengwa kwa ajili ya machinga. Maelekezo niliyomwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji masoko hayo yawe na miundombinu inayowezesha wafanyabiashara na yawe yanafikika kwa urahisi na wanunuzi jambo ambalo ni muhimu kwa wafanyabiashara,” amesema Mkude.

Kufuatia hatua hiyo, Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Ahmed Jamal alitangaza kusitisha mgomo huo kupisha mazungumzo yaliyoitishwa na Mkude ambayo anaamini yataleta muafaka wa kudumu.

“Tumepokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya kuwapo mazungumzo ya kina yenye lengo la kutupa wafanyabiashara wote fursa ya haki ya kutafuta riziki kwa njia halali, natangaza kusitisha mgomo kwa sasa kupisha mazungumzo,” amesema Jamal.

Baada ya mkutano wa Mkude na wawakilishi wa wafanyabiashara na viongozi wa masoko jijini Arusha, amesema Serikali imeshaweka miundombinu rafiki ya kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo kufanya shughuli zao kwenye maeneo yaliyotengwa na sio mbele ya maduka na kando ya barabara.

Amesisitiza wafanyabiashara wenye maduka wapo kihalali na wanalipa kodi hivyo shughuli zao hazipaswi kuwekewa vikwazo kwa sababu machinga wanayo maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao lakini hawayatumii.

Mkude ametoa siku tatu kwa machinga kuacha mara moja kupanga bidhaa zao mbele ya maduka ya wafanyabiashara na pembezoni mwa barabara, na kuwataka kwenda katika maeneo waliyopewa na halmashauri ya jiji.

“Nataka tuwe na mji unaozingatia mipango miji ambao unapitika badala ya hali ya sasa kila mfanyabiashara kufanya lake, nimepiga marufuku wenye maduka kuweka bidhaa zao nje ambayo ni maeneo ya watembea kwa miguu kwa sababu inahatarisha usalama wa watembea kwa miguu ambao wanalazimika kupita barabarani,” amesema Mkude.

Kuhusu wenye maduka waliopanga bidhaa zao kwenye njia za watembea kwa miguu amewapa siku saba wawe wameondoa bidhaa zao kabla Serikali haijachukua hatua za kisheria.