Hali tete kambi ya Nyarugusu, huduma muhimu zaondolewa

Kasulu. Wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wanaohifadhiwa kwenye kambi ya Nyarugusu Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wanakabiliwa na hali ngumu ndani ya kambi hiyo baada ya kupungua kwa huduma za kijamii kwa asilimia 50, hatua inayowafanya kutaka kurudi nchini kwao.

Akitoa taarifa hiyo leo Januari 14, 2026 kwa ujumbe wa mawaziri wa serikali ya DRC  na Tanzania waliotembelea kambi hiyo na kuzungumza na wakimbizi hao. Kaimu Mkuu wa kambi hiyo, Samuel Kuyi amesema hatua hiyo imekuja baada ya mashirika ya kuhudumia wakimbizi kukumbwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha.

Amesema wakimbizi hao wamekumbwa na changamoto ya upungufu wa chakula kutoka wastani wa asilimia 75 hadi kufikia asilimia 65 ambapo kinachotolewa kwa sasa hakikidhi mahitaji, ambapo kila mkimbizi anapata kilo 9.5 za chakula kwa mwezi.

Kuyi amesema kwa upande wa huduma za afya kwa sasa kimebaki kimoja kinachotoka huduma vingine vikiwa vimefungwa, huku huduma za rufaa kwenda Hospitali ya Mkoa au kanda Bugando zimeondolewa.

Baadhi ya wakimbizi kutoka DRC waishio katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma wakisikiliza mkutano wa viongozi kutoka nchini DRC waliowatembelea kambini humo.

“Kambi hiyo yenye jumla ya wakimbizi 132,404, huku wa kutoka DRC wakiwa 86,918, wa Burundi wakiwa 45,346 na   wa mataifa mengine wakiwa 98 hivyo kukosa huduma za afya kambini kumesababisha ongezeko la idadi ya vifo,”amesema Kuyi.

Amesema taratibu za wakimbizi wa DRC kwenda nchi ya tatu Marekani, Canada na Ulaya zimezuiwa na hata taratibu za masomo kwa wakimbizi hao kwa sasa zimesimama, baada ya mashirika yanayoshughulikia masuala ya elimu kujiondoa.

Akieleza kuhusu hali ya elimu kambini humo, Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania, Sudi Mwakibasi amemuomba Waziri wa Nchi Wizara ya Masuala ya Jamii, Hatua za Kibinadamu na Mshikamano wa DRC, Eve Bazaiba Masudi kuiomba serikali ya nchi hiyo kugharamia elimu kwa wakimbizi hao, ili waweze kuendelea na masomo kwa mitaala ya nchini mwaoa na kufanya mitihani ya taifa.

Naye Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya amesema pamoja na wakimbizi hao kuomba hilo kwa hiari,  hakuna mkimbizi wa DRC atalazimishwa kurudi nchini mwao bali suala la usalama na utu wa wakimbizi hao utazingatiwa kama ilivyo kwa wale wa Burundi ambao kwa sasa wanasaidiwa kurudi nchini kwao kwa hiari.

Akizungumza katika Mkutano na wakimbizi kambini hapo, Waziri wa DRC Masudi amesema bado maeneo mengi wanayotoka wakimbizi hao hayana amani na hivyo siyo rahisi kuwarudisha huko. “Tunawatafutia maeneo yenye  amani wakimbizi wanaotaka kurejea Congo kwa sasa, ila wanakotoka walio wengi hakuna amani.”

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Barbara Dotse amesema shirika hilo linaendelea kutafuta fedha ili huduma za kibinadamu kwa wakimbizi hao wa DRC ziweze kurejea kawaida, huku wakitafuta suluhisho la kudumu la wakimbizi hao kurejea nchini mwao.

Nao baadhi ya wakimbizi wa DRC wamesema wako tayari kurejea nchini kwao kwa hiari endapo serikali yao itaimarisha usalama na amani katika maeneo yenye machafuko nchini humo.

“Kutokana na hali ilivyo kwa sasa ndani ya kambi kukosa huduma muhimu za kijamii tupo tayari kurudi nchini kwetu kwa hiari yetu, tumekosa uhuru hata wa kufanya biashara ili kuweza kupata hata fedha kidogo kwa ajili ya kujikimu mahitaji yetu, hivyo suluhisho ni kurudi kwetu na kwenda kujitegemea,”amesema Apolina Msumbuko.