MICHAUNO ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 ipo hatua nusu fainali, huku ni nyota mmoja tu wa Ligi Kuu Bara akisalia Morocco, kipa wa Nigeria anayekipiga Singida Black Stars, Amas Obasogie baada ya Djigui Diarra kung’oka akiwa na Mali, lakini kuna kocha mmoja ameshindwa kujizuia kwa kipa huyo wa Yanga.
Kocha wa zamani wa Simba Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema Diarra ni mwamba sana na ni mmoja ya wachezaji wanayoipa jeuri Yanga katika michuano ya ndani na hata kimataifa kwani anajua kujituma uwanjani.
Diarra ameaga michuano ya AFCON inayoendelea Morocco akiwa ametumika kwa dakika zote 570 za mechi tano ilizocheza Mali, akifanya jumla sevu kubwa 16 akiwa na clean sheet moja, huku akiokoa penalti mbili licha ya kuruhusu mabao matatu na timu hiyo ya taifa ikishindwa kupata ushindi wowote ndani ya dakika 90.
Kiwango alichokionyesha katika michuano hiyo ikiwamo kuwa Nyota wa Mchezo katika mechi ya 16 Bora dhidi ya Tunisia huenda kikaongeza thamani yake sokoni ukizangatia kwamba amesalia na mkataba wa mwaka mmoja tu na kikosi cha Yanga aliyojiunga nayo tangu mwaka 2021 akitokea Stade Malien ya Mali.
Akizungumza na Mwanaspoti, Robertinho ametamka maneno ya heshima kwa ubora wa Diarra akisema kama kuna nguzo muhimu katika kikosi cha Yanga basi ni uwezo wa kipa huyo ambaye hata akiwa uso na lango lake bado hauna uhakika wa kufunga bao hadi liingie wavuni.
Robertinho alisema, Diarra amethibitisha ni kipa wa daraja kubwa kutokana na namna alivyofanya kazi kubwa kuibeba Mali ambapo ubora wake ulikuwa silaha muhimu kwa timu yake kutopoteza kirahisi mechi zake.
Kocha huyo alisema uwepo wa Diarra ni kielelezo kingine cha kwamba Yanga ina timu bora ambayo inastahili kuendelea kufanya makubwa kutokana na kusajili wachezaji wenye viwango vya juu kuliko wapinzani wao wengine.
“Kitu kilichonivutia sana katika hizi fainali ni kuwaona wachezaji ambao nilikuwa nakutana nao wakati nafanya kazi Simba, mchezaji aliyecheza kwa kiwango kikubwa sana ukiniuliza ni huyu Diarra ni kipa wa kiwango cha juu sana,” alisema Robertinho na kuongeza;
“Mali wana timu nzuri na wachezaji wazuri, lakini ukiangalia kwa utulivu utagundua kufika kwao robo fainali ni kazi kubwa ya huyu golikipa, amekuwa na muendelezo wa kiwango bora sana. Unapomuona Diarra unapata majibu kwamba timu ya Yanga inastahili kupata mafanikio kwani kuna wachezaji wengi bora nadhani timu zingine zinatakiwa kujifunza kuanzia hapo.”
Umahiri wa Diarra ulichangia kumponza Robertinho kutimuliwa Simba baada ya kichapo cha mabao 5-1 katika Dabi ya Kariakoo ya Novemba 5, 2023 licha ya kupata ushindi wa mabao 2-0 kabla ya mechi hiyo timu hizo zilipofunga msimu wa 2022-2023 Aprili 16, 2023 kwa mabao ya Henock Inonga na Kibu Denis.
Kocha huyo Mbrazili, pia alimzungumzia beki Fondoh Che Malone ambaye naye ameishia hatua ya robo fainali, akisema Simba inatakiwa kusikitika kwa kupoteza mchezaji bora kama huyo ambaye tangu ameondoka Tanzania amekuwa kwenye kiwango bora.
“Ligi ya Algeria ni ngumu sana, lakini unaona Che Malone ameendelea kufanya vizuri, angalia kwenye timu yake ya taifa ya Cameroon amekuwa na kiwango bora utasema na yeye anacheza Ulaya, wakati unajenga timu imara alafu ukapoteza mchezaji bora kama huyu ni lazima ujiangalie mara mbili juu ya maamuzi yako,” alisema Robertinho aliyepo Jeddah SC ya Saudi Arabia na kuongeza;
“Simba wangekuwa wanajivunia kuwa na beki bora kama Che Malone lakini naamini na wao wanaumia kama mimi kuona anafanya vizuri lakini akiwa ameondoka kwenye timu yako, nilikwambia sioni beki imara wa kati pale Simba kumshinda Che Malone, ni kamanda muhimu uwanjani.”
