Kenya. Ikiwa ni chini ya saa 24 baada ya serikali ya Uganda kuzima huduma ya intaneti kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho, wasafirishaji mizigo katika Bandari ya Mombasa wamelazimika kusitisha huduma.
Mawakala wa usafirishaji mizigo wamesema uamuzi wa mamlaka za Uganda wa kuweka zuio la kitaifa la intaneti umevuruga mawasiliano kati yao na madereva, pia umeathiri ufuatiliaji nyaraka na utoaji wa mizigo.
Mwenyekiti wa Chama cha Usafirishaji na Uhifadhi Mizigo Kenya (Kifwa), Fredrick Aloo amesema sekta ya usafirishaji inategemea intaneti na mizigo haiwezi kutolewa kupelekwa mahali popote bila mawasiliano.
“Sekta ya usafirishaji inategemea upatikanaji wa intaneti. Hivyo iwapo intaneti imesitishwa, uratibu umekuwa mgumu, ufuatiliaji na uwasilishaji wa nyaraka,” amesema Aloo.
Kwa mujibu wa mawakala wa mizigo, wamesema kuzimwa kwa intaneti kumeathiri mawasiliano na madereva na wateja kupitia WhatsApp, ujumbe mfupi na Telegram.
Aloo amesema mizigo ya kupita transit hutegemea GPRS inavyotuma taarifa kupitia data ya simu na intaneti ya umma, ambavyo sasa vimeathirika.
“Utoaji wa mizigo umeathirika kwa sababu baadhi ya mifumo ya forodha na usafirishaji hutegemea intaneti. Kukosekana kwa intaneti kunaweza kusababisha msongamano mkubwa katika vituo vya mipakani,” amesema Aloo.
Jana Jumanne, mamlaka ya udhibiti mawasiliano nchini Uganda iliwaagiza watoa huduma ya mitandao ya simu kuzuia upatikanaji wa intaneti ya umma hatua iliyoanza kutekelezwa kuanzia saa 12 jioni.
Mfanyabiashara wa Mombasa, Roy Mwanthi amesema kwa sasa anatarajia kushughulikia kusambaza mizigo ya ndani hadi uchaguzi utakapomalizika na kuondolewa zuio la kusitisha huduma ya intaneti.
“Mizigo ambayo tayari imeshasafirishwa itasubiria mipakani ya Busia na Malaba, lakini ili kuhakikisha usalama na kuepuka hasara, tutajikita kusafirisha mizigo ya ndani,” amesema Mwanthi.
Awali, Mamlaka ya Mawasiliano ya Uganda iliwapa taarifa wananchi kwamba watoa huduma wote wangesitisha huduma za intaneti kabla ya uchaguzi mkuu.
Uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika kesho Alhamisi, Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 81, anapambana na mpinzani wake Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine mwenye umri wa miaka 43.
Hata hivyo, mamlaka hiyo imetetea uamuzi huo kwa misingi ya usalama wa umma, ikisema unalenga kuzuia taarifa potofu mtandaoni, upotoshaji wa habari, udanganyifu wa uchaguzi, pamoja na kuchochea vurugu.
Katika barua yake kwa waendeshaji wa mitandao ya simu, Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) ilieleza sababu za uamuzi huo ni kufuatia pendekezo kutoka kwa vyombo vya usalama, likiwemo Jeshi na Polisi.