Ligi Kuu Bara kuaanza na viporo

LIGI Kuu Bara iliyosimama tangu Desemba 7, mwaka jana kupisha michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2025) na Kombe la Mapinduzi 2026, inarejea kesho Ijumaa kwa mechi mbili za viporo.

Ligi hiyo ilipangwa kuendelea Januari 21, mwaka huu, lakini kwa mujibu wa marekebishoi madogo ya mechi ambazo hazipigwa huko nyuma ni kwamba sasa ligi itaanza keshokutwa ikiwa ni baada ya kusimama karibu siku 40.

Michuano hiyo inarejea ambapo mabingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu, Yanga wataanza kufungua pazia hilo kwa kucheza na JKT Tanzania ikiwa ni mechi ya kiporo itakayopigwa kuanzia saa 10:00 za jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Yanga ndio timu ya mwisho kucheza Ligi Kuu Bara kabla ya kusimama na kupisha timu ya taifa ya Taifa Stars kujiandaa na michuano ya Afcon, ambapo kikosi hicho kilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kikiwa ugenini Desemba 7, 2025.

Mechi nyingine itakayopigwa kesho saa 1:00 usiku, itakuwa kati ya Dodoma Jiji inayoshika nafasi ya 15 na pointi sita itakapoikaribisha Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

LIG 01

Baada ya hapo ligi hiyo itaendelea Jumamosi, ambapo Azam iliyokosa taji la Mapinduzi kwa kuchapwa na Yanga kwa penalti 5-4 baada ya suluhu ndani ya dakika 120 itaikaribisha Coastal Union saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Kocha wa Simba, Steve Barker, aliyejiunga na kikosi hicho Desemba 19, 2025 akirithi mikoba ya Dimitar Pantev ataanza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar Jumapili saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Simba iliyopo katika nafasi ya tano na pointi 12 inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu mbaya baada ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuchapwa mabao 2-0 na Azam, Desemba 7, 2025.

LIG 02

Jumatatu ya Januari 19, 2026 ligi itaendelea ambapo Yanga itakuwa KMC Complex, Dar es Salaam kucheza dhidi ya maafande wa Mashujaa kutoka Kigoma katika mechi itakayopigwa kuanzia saa 10:00 za jioni.

Mechi za mwisho za viporo, zitapigwa Jumanne, Januari 20, 2026, ambapo Azam itaikaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 10:00 jioni, huku Singida Black Stars ikicheza na JKT Tanzania saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Siku inayofuata yaani Januari 21 ngwe ya ligi hiyo inayoongozwa kwa sasa na JKT Tanzania itaendelea kama ilivyopangwa na Bodi ya Ligi (TPLB) ambayo ilifanya marekebisho kidogo kwa mechi za Januari 20 ambazo awali zilikuwa zikionekana zitapigwa siku hiyo.