Dar es Salaam. Kauli za mara kwa mara za Rais Samia Suluhu Hassan kukemea mivutano kati ya watumishi na wateule wake zimeendelea kuwa rejea ya mjadala wa utendaji wa Serikali, huku wachambuzi wa siasa na uongozi wakisema ili kumaliza changamoto hiyo, watendaji wanapaswa kujengewa uelewa.
Ingawa Rais amekuwa akitoa onyo na maelekezo kwa nyakati tofauti, hali ya misuguano miongoni mwa baadhi ya watendaji bado inaonekana kujitokeza.
Hali hiyo ilishuhudiwa hata katika awamu zilizopita za uongozi, ikiwamo ya hayati Rais John Magufuli, aliyewahi kukemea tabia ya migongano na malumbano miongoni mwa viongozi wa Serikali, akisisitiza mshikamano na uwajibikaji kama msingi wa ufanisi wa utawala.
Mfano wa karibuni wa msimamo huo ulijitokeza Januari 13, 2026, wakati Rais Samia alipowaapisha mawaziri na mabalozi wapya Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.
Katika hafla hiyo, alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda na Naibu wake, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), kuacha malumbano, badala yake kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.
Alisema hatasita kuwaweka kando viongozi watakaoshindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na migogoro ya ndani, akisisitiza kuwa Serikali yake inahitaji utendaji, si migongano.
Kauli hiyo imeamsha kumbukumbu za matamko mengine ya Rais Samia katika vipindi tofauti akilaani tabia ya mivutano miongoni mwa wateule wake.
Mfululizo huo wa kauli unaibua swali kuhusu chanzo cha tatizo hilo na kwa nini licha ya maelekezo ya viongozi wa juu, bado linaendelea kujitokeza.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya siasa na uongozi, suluhisho la kudumu halipo tu katika onyo au hatua za kinidhamu, bali katika kuwajengea wateule uelewa mpana wa misingi ya uongozi, maadili ya utumishi wa umma na matumizi ya busara katika kushughulikia tofauti za kimtazamo.
Kwa mtazamo huo, wachambuzi wanaeleza endapo wateule watajengewa uwezo wa kutofautisha kati ya masuala binafsi na wajibu wa ofisi wanazoshika, pamoja na kuimarishwa kwa utamaduni wa majadiliano ya ndani, mivutano itapungua na utendaji wa Serikali utaimarika.
Februari 2023, Rais Samia akiwaapisha mawaziri, naibu mawaziri, mkuu wa mkoa, pamoja na makatibu wakuu na naibu wao, Ikulu ya Chamwino, Dodoma alisema imefikia hatua waziri na naibu wake au katibu mkuu na naibu wake hawaelewani, jambo linaloathiri utendaji wa Serikali.
Kwa wakati huo, alisema mvutano huo umejitokeza zaidi kati ya mawaziri na naibu wao, pamoja na makatibu wakuu na naibu wao. Alionya kuwa, safari ijayo wote wawili watawajibishwa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Vilevile, Mei 2023, Rais Samia alieleza sababu ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Kabidhi Wasii Mkuu katika Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Angela Anatory na nafasi yake akimteua Frank Kanyusi.
Alieleza uwepo wa ugomvi usiokwisha baina ya Kabidhi Wasihi Mkuu na Naibu wake, Lina Sanga, ulioshusha utendaji kazi. Samia alimteua Irene Lesulie kuwa Naibu Kabidhi Wasii Mkuu.
“Kabidhi Wasii Mkuu na naibu wako nimewateua baada ya kuwaondoa viongozi wote wawili waliokuwepo pale, nilikuwa nategemea wananchi wapate huduma za kuridhisha ndani ya ile ofisi, lakini kilichokuwa kinatokea ilikuwa ni ugomvi.
“Nikasema labda kwa kuwa wote walikuwa kinamama ndiyo maana kulikuwa na ugomvi mkubwa, lakini ukiangalia kwa ndani kulikuwa na kutokutekelezeka kwa kazi vizuri, mwingine akisema huyu anakasirika, mwingine akirekebisha mwingine anachafua, kwa hiyo nikaamua kuwaondoa wote wawili watapangiwa kazi nyingine, sasa nendeni ninyi,” aliagiza.
Katika halmashauri, mgogoro wa wateule wa Rais ulijitokeza katika utawala wa awamu ya tano kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Sada Malunde na aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Wende Ng’ahara.
Februari 20, 2019 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ziarani mkoani Kagera aliwataka viongozi hao wamalize tofauti zao.
“Mkurugenzi unagombana na DC wako, DAS nawe umeingia kwenye mgogoro, mnagombana mpaka mnatumiana uchawi,” alisema na kuongeza:
“Mmeanza kuhama na ofisi, mtakimbia wilaya. Mnagombana nini? Ninyi viongozi mnashindwa kukaa na kumaliza mambo hayo? Ninazo habari zote za migogoro yenu, halafu mnagombana wakubwa, wadogo wapo wanaangalia, ni vituko, badilikeni.”
Wakati wa utawala wake, Rais Magufuli aliwahi kuzungumzia migogoro kwa viongozi aliowateua akieleza:
“Pale Dodoma, mkurugenzi wa jiji na DC walikuwa wanagombana, nika-send message (nikatuma ujumbe) kwamba ‘endeleeni kugombana tu, mtagombania vijijini siku moja. Wamenyamaza naona yameisha.”
Desemba 31, 2019, akizungumza na askari wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Dk Magufuli aliwazungumzia wateule wake wa Wizara ya Maliasili akiwataka kuelewana lasivyo atatengua uteuzi wao.
Alitoa siku tano kuanzia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Dk Hamisi Kigwangalla na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda kuondoa tofauti zao vinginevyo atatengua uteuzi wao.
“Ninafahamu watendaji wenu wa juu, katibu mkuu na waziri kila siku wanagombana na ninawatazama taratibu, nilishampa kazi Katibu Mkuu Kiongozi awaite awaeleze lakini wasipobadilika nitawaondoa,” alisema.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 14, 2026, mchambuzi wa masuala ya siasa na uongozi, Profesa Ali Makame, amesema jambo la msingi katika kumaliza changamoto za wateule wa Rais ni kujengewa uelewa.
Amesema viongozi wanapoteuliwa kila mmoja anakuwa na mtazamo wake, huku madaraka huambatana na nguvu na busara.
“Inapotokea ikabakia moja, hali haitakuwa nzuri, sasa wateule wanapaswa kupatiwa uelewa kwamba kazi hii ni dhamana inayokwenda na nguvu uliyopewa na busara,” amesema na kuongeza:
“Busara ndiyo asilimia kubwa tunayoitumia kwa sababu unapopewa dhamana inaambatana na sheria, ambayo haitakuambia ni busara gani utaitumia kwenye mazingira tofauti ya kazi.”
Profesa Makame amesema mtu anapotumia sheria pekee huleta mabavu, ambayo yanapotengenezwa huleta kiburi.
Amesema jambo baya viongozi wanaopewa dhamana wanashindwa kutofautisha mamlaka na busara, hivyo hutumia mamlaka pekee ambayo ndiyo chanzo cha mivutano.
Amesema busara inapowekwa kando hali ya kutunishiana misuli huibuka na kila mtu kujiona anafaa zaidi ya mwingine.
“Hii inachangiwa zaidi na umri, si kosa wala siyo dhambi kuwa na viongozi wenye umri mdogo, lakini hivi sasa kuna kutambiana katika hali ya kawaida ya maisha. Kijana anamtambia mwenzake kwa mafanikio ya maisha yake mali alizonazo au mahusiano yake kwamba yeye ana mzuri kuliko mwingine,” amesema.
Profesa Makame amesema ni muhimu jambo hilo kuangaliwa hata kutoa mafunzo maalumu kwa wateule, akikumbusha kuwa, miaka ya nyuma utaratibu huo ulikuwapo wa kuandaa viongozi.
Amesema wapo wanaojikuta wapo kwenye uongozi bila kupatiwa mafunzo kitendo ambacho huwapa fikra kuwa nafasi hiyo ameipata kwa uwezo wake na hakuna anayeweza kumkemea wala kumshauri.
“Tukiwa na utaratibu wa kuwapa wanaoteuliwa ABC ya kitaaluma au uzoefu inaweza kupunguza changamoto na mivutano baina ya viongozi,” amesema.
Katika mtazamo wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Mwalimu Samson Sombi amesema ili kumaliza tatizo hilo lazima kuwe na heshima ya mipaka ya madaraka kwa kila nafasi ya uongozi.
“Viongozi wanapaswa kupimwa kwa matokeo ya pamoja badala ya mafanikio binafsi, jambo litakalopunguza mashindano yasiyo na tija na kuongeza mshikamano kazini,” amesema.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Hery Mkunda amesema migogoro baina ya watendaji wa Serikali mara nyingi hutokana na mambo binafsi.
Ameeleza utumishi wa Serikali ni tofauti na sekta binafsi, kwani ndani ya umma majukumu ya watendaji wote yameainishwa.
“Linapokuja suala la migogoro kwa watendaji mingi ni binafsi, mtu anaona kwa nini huyu ananipeleka hivi wakati sisi wote ni wateule,” amesema.
Mkunda amesema wakati mwingine kwa kuwa waziri ndiye msemaji mkuu wa wizara, katibu mkuu anapofanya jambo bila kumshirikisha huibua mzozo kati ya wawili hao.
Mzozo huo amesema hutokana na mmoja kuona amedharauliwa, hivyo kuibua mgongano baina ya watendaji hao wawili.
Amesema kinachohitajika ni busara kwa kuwa matatizo mengine ni binafsi na siyo ya kitaasisi.
