Dar es Salaam. Serikali kwa kushirikiana na Jamhuri ya Korea imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kisasa wa kuboresha mfumo wa majitaka, unaolenga kukabiliana na changamoto sugu ya majitaka katika miji ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mbali na mkakati huo, ushirikiano wa mradi huo unaolenga ongezeko la matumizi ya majisafi linalotarajiwa katika majiji hayo kwa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma na maji ya Mto Rufiji hadi Dar es Salaam, ili kuongeza mahitaji ya huduma hiyo.
Akizungumza jijini Dodoma leo Jumatano, Januari 14, 2026 baada ya mazungumzo na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Ahn Eunju, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema ushirikiano huo utaimarisha kwa kiasi kikubwa huduma ya majitaka kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, Dodoma na maeneo ya jirani.
Waziri Aweso amesema mradi huo mkubwa kwa sasa unatekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Kinondoni, utekelezaji wake umefikia asilimia 10.8.
“Mradi huo unalenga kuboresha mfumo wa uondoshaji na uchakataji wa majitaka yanayotokana na matumizi ya maji safi ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka,” amesema.
Ameeleza mradi huo unahusisha ujenzi wa Mtambo wa Kisasa wa kuchakata majitaka katika eneo la Buguruni, maarufu kama Mabwawa ya Majitaka Buguruni na kuachana na mfumo wa zamani wa mabwawa ya wazi yaliyokuwa karibu na makazi ya wananchi.
“Hatua hiyo inatarajiwa kuboresha usafi wa mazingira na kuondoa athari za kiafya kwa wakazi wa eneo hilo,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri Aweso, mradi huo unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa ya mlipuko yaliyokuwa yakiwakabili wananchi wa Buguruni na maeneo ya jirani, pamoja na kupunguza gharama za uondoshaji wa majitaka, hususan kwa wakazi wa katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Pia amesema Serikali za Tanzania na Korea zinatekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Usafi wa Mazingira katika Jiji la Dar es Salaam wenye thamani ya takribani dola za Kimarekani milioni 90. Mradi huo, unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi milioni 1.8.
Katika mazungumzo kati ya Waziri Aweso na Balozi Eunju yalijikita pia katika kuimarisha ushirikiano wa sekta ya maji, ikiwemo huduma ya majisafi, usafi wa mazingira, usalama wa maji, rasilimali za maji, majitaka, uvunaji wa maji ya mvua pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Balozi Ahn Eunju amempongeza Waziri Aweso kwa juhudi kubwa anazozifanya katika sekta ya maji na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Majitaka Buguruni.
Amesisitiza dhamira ya Korea kuendelea kushirikiana na Tanzania, hususan katika eneo la usalama wa maji, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la mahitaji ya huduma za maji.