BAADA ya kufunga mabao matano katika mechi ya jana dhidi ya Fountain Gate Princess, mshambuliaji wa Yanga Princess, Jeanine Mukandayisenga amevunja rekodi ya msimu uliopita ya kufunga mabao 13.
Nyota huyo raia wa Rwanda katika mechi hiyo ya jana ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-4 aliweka kambani mabao yote na kuipa pointi tatu mabinti hao Wananchi iliyowafanya waendelee kusalia nafasi ya pili ya msimamo wa WPL.
Katika msimu wa kwanza kwenye ligi hiyo, Mukandayisenga alifunga mabao 12 kwenye mechi tisa alizocheza akiwa amejiunga na Wananchi wakati wa dirisha dogo akitokea Rayon Sports ya Rwanda.
Mechi ya jana ilimfanya mchezaji huyo avunje rekodi ya msimu uliopita alipofikisha mabao 13 na kuongoza kwenye mbio za ufungaji bora.
Nyota huyo amekuwa na mwendelezo mzuri wa kutupia kambani mabao na matatu aliyofunga (hat-trick) jana inakuwa ya pili kufunga msimu huu akiendelea kuiweka kwenye nafasi nzuri Yanga Princess.
Akizungumzia mwendelezo huo, Mukandayisenga amesema: “Namshukuru Mungu kwa kuwa na mwendelezo, lakini pongezi ziende kwa wachezaji wenzangu. Pili natamani niendelee kufunga kwa sababu ni kazi yangu na kuisaidia timu.”
Mchezaji huyo hadi sasa ndiye kinara wa ufungaji katika ligi hiyo akifuatiwa na Winifrida Gerald wa JKT mwenye mabao saba, Jentrix Shikangwa na Aisha Mnunka wa Simba Queens wakiwa nayo sita sita, huku Aregash Kalsa wa Yanga Princess akitupia matano.
Stumai Abdallah wa JKT Queems aliyeibuka mfungaji bora msimu uliopita hadi sasa amefunga bao moja na asisti nne, ilhali uliopita hadi sasa alikuwa na mabao 11.
