Museveni ahitimisha kampeni, ahimiza wananchi kujitokeza kupiga kura kesho

Uganda. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amehitimisha kampeni zake katika mkutano uliofanyika Kampala, huku akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupiga kura kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika kesho Alhamisi.

Mkutano huo wa kuhitimisha kampeni uliofanyika jana Jumanne Januari 13, 2026, wananchi na wafuasi wa chama chake walijitokeza kusikiliza sera za Chama cha National Resistince Movement (NRM) jijini Kampala.

Katika hotuba yake ya kufunga kampeni, Museveni amewahimiza wafuasi wake kupiga kura, akionya kuwa jaribio lolote la kuharibu uchaguzi litadhibitiwa.

Kiongozi huyo mwenye miaka 81 ameiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1986, na hivi sasa anawania muhula wa saba madarakani akichuana na mpinzani wake Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine anayegombea kupitia Chama cha National Unity Platform (NUP), anayeungwa mkono na vijana wengi nchini humo.

Akiwa mmoja wa marais wakongwe zaidi barani Afrika, serikali yake imebadilisha katiba mara mbili ili kuondoa vikwazo vya umri na idadi ya mihula, jambo lililomwezesha kugombea tena katika uchaguzi.

Picha kutoka mojawapo ya mikutano ya kampeni ya Yoweri Kaguta Museveni anayewania kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Uganda katika uchaguzi utakaofanyika Januari, 2026. Picha na Mitandao

Hata hivyo, licha ya umri wake mkubwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa, ukiukwaji wa haki za binadamu, na kashfa za ufisadi katika serikali yake, wafuasi wake bado wamesimama imara kumuunga mkono.

Mwanachama wa NRM, Emma Akello, amesema amefurahishwa na programu za vijana zilizoanzishwa na Museveni, lakini akaongeza kuwa fedha zaidi zinapaswa kuelekezwa kwa watu maskini zaidi.

“Rais amewekeza fedha nyingi kwa ajili ya vijana,” amesema.

“Lakini watu walioko katika ofisi hizo wanapaswa kutafuta njia bora zaidi za kuhakikisha fedha hizo zinawafikia vijana, hasa vijana wa mitaani. Hawapati fedha hizo kwa sababu ya usimamizi mbaya,” amesema.

Mfuasi mwingine wa NRM, Gloria Ninsiima, amesema kuwa chini ya uongozi wa Museveni, haki za wanawake zimezingatiwa katika maeneo mbalimbali nchini humo.

“Tangu Museveni aingie madarakani, sisi wanawake tulioolewa. Zamani tulifungiwa jikoni, lakini sasa tunaweza kuzungumza hadharani,” amesema.

Mamlaka za Uganda zimeanza kupeleka wanajeshi katika maeneo mbalimbali ya Kampala tangu Jumamosi, huku magari ya kulinda usalama yakisambazwa katika maeneo mbalimbali ya za jiji la Kampala.

Tume ya Mawasiliano ya Uganda  jana Jumanne imeagiza watoa huduma za intaneti ya simu kusitisha huduma kwa muda, ikitaja sababu za kusambaa taarifa za upotoshaji, udanganyifu wa uchaguzi na uchochezi wa vurugu.

Wapinzani wa Museveni katika kinyang’anyiro cha urais, akiwemo mwanasiasa mwenye umri wa miaka 43 na nyota wa muziki aliyebadili taaluma, anayejulikana kama Bobi Wine, nao pia wamefanya mikutano ya kampeni.

Picha kutoka mojawapo ya mikutano ya kampeni ya Yoweri Kaguta Museveni anayewania kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Uganda katika uchaguzi utakaofanyika Januari, 2026. Picha na Mitandao

Kiongozi huyo wa upinzani, aliyewahi kumpinga Museveni katika uchaguzi wa mwaka 2021, amekuwa akifanya kampeni akiwa amevaa koti la kujikinga na risasi pamoja na kofia ya chuma ili kujilinda dhidi ya mashambulizi ya silaha za moto.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imesema kuwa uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya ukandamizaji na vitisho, huku mamlaka zikiwakamata mamia ya wafuasi wa upinzani.