Profesa Mbarawa: Ifikapo Mei ndege zianze kutua Msalato

Dodoma. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amemwagiza mkandarasi anayejenga uwanja wa ndege wa Msalato kukamilisha kazi yake ili ifikapo  Mei ndege zianze kutua.

Aidha Profesa ameitaka pia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuanza mchakato wa kutafuta magari ya zimamoto walau matatu kwa maeneo mengine, wakati magari matano ya uwanja huo yakitaraji kufika Agosti hadi Desemba mwaka huu.

Waziri Mbarawa ametoa maagizo hayo leo Jumatano Januari 14,2026 alipozungumza baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato unaojengwa nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Ujenzi wa uwanja huo ulianza Aprili 20,2022 na ulitarajia kukamilika Aprili 18,2025 ila waliomba muda wa nyongeza hadi Februari 21,2026 lakini wameomba muda zaidi kukamilisha baadhi ya maeneo ili kufanya umaliziaji.

Amesema uwanja huo ambao unajengwa kwa zaidi ya Sh370 bilioni fedha kutoka mkopo nafuu wa Benki ya Afrika na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo ni M/s Sinohydro Corporation Ltd kwa kushirikiana na M/s Beijing Sino-Aero Construction Engineering Co Ltd.

“Maendeleo ya ujenzi wa uwanja huu siyo mabaya, lakini nataka kwenye umaliziaji kuonyesha thamani halisi ya fedha, nataka isizidi mwezi wa tano uwanja uanze kupokea ndege hakuna namna ya kuchelewa tena,” amesema Mbarawa.

Ameagiza pia mifumo ya uwekaji mafuta kwenye ndege iangaliwe kwani duniani kote ujazaji mafuta kwenye ndege haujazwi kwa kutumia magari.

Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa (Katikati) akitoa maagizo ya kukamilika haraka ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Msalato Dodoma.

Katika eneo la ujenzi wa jengo la abiria umefikia asilimia 67 wakati eneo la kuruka na kutua ndege ujenzi wake umefikia asilimia 97.

Mkurugenzi wa uwanja wa ndege wa Msalato, Clemence Jingu amesema Serikali imeshapeleka watumishi 170 katika uwanja huo mpya na wako tayari kwa kazi hata ndege zikianza kutua wakati wowote.

Jingu amesema miundombinu ya uwanja huo ipo tayari kwa sehemu kubwa ukibakiza mapungufu machache ikiwemo eneo la ujazaji mafuta ambalo linatakiwa kuwa la kisasa.

Kuhusu magari ya zimamoto, Jingu amesema mkandarasi ameshaagiza na kinachosubiriwa ni muda tu lakini haitazidi Oktoba mwaka huu.

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanrods), Zuhura Aman amesema maeneo mengi yanayojengwa ndani ya uwanja yamefikia hatua nzuri.

Zuhura ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili ni ujenzi wa mfumo wa usambazaji mafuta eneo la maegesho, kujenga bwawa la kuhifadhia maji ya mvua kwa sababu za kimazingira, ili kutumia kwenye umwagiliaji na ujenzi wa barabara ya kiungio na maegesho ya ndege.