WAKATI Jumanne ya Januari 13, 2026 ikipigwa fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kati ya Azam dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, kilio kimeendelea kusikika kutokana na wenyeji timu za Zanzibar kushindwa kutoboa.
Michuano hiyo iliyoanza Desemba 28, 2025 kwa kushirikisha timu kumi ikianzia kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja hatua ya makundi na nusu fainali kisha fainali kupigwa Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, wenyeji kwa maana ya timu za Zanzibar zimeishia makundi ikiwamo bingwa mtetezi, Mlandege iliyomaliza bila pointi ikiwa ndio pekee iliyoondoka patupu.
Hali hiyo imemfanya Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ali Abdulghulam Hussein kutaja sababu ya hayo yote akisema imetokana na timu za Bara kuwa na maandalizi mazuri na uwekezaji mkubwa tofauti na zile za Zanzibar.
“Timu za Tanzania Bara zinajiandaa vyema na zinatumia haya mashindano kwa maandalizi makubwa ya kombe la Afrika, hii imeonyesha wamekuja kwenye kazi kwelikweli.
“Hata uwekezaji wao ni mkubwa ndio maana hata timu zetu hazifanyi vizuri, lakini mipango kama wizara tutahakikisha tunazisaidia klabu zetu kadiri inavyowezekana na wao waingie kiushindani,” amesema kiongozi huyo.
Timu zilizoshiriki Kombe la Mapinduzi 2026 ni Mlandege, Fufuni, KVZ na Muembe Makumbi City kutoka Zanzibar. Azam, Yanga, Simba, Singida Black Stars na TRA United za Tanzania Bara huku URA ikitokea Uganda.
Baada ya kumalizika hatua ya makundi, timu nne za Tanzania Bara zilifuzu nusu fainali ambazo ni Azam, Yanga, Singida na Simba. Timu hizo pia ndizo zinaiwakilisha Tanzania kimataifa zikiwa hatua ya makundi, Yanga na Simba zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam na Singida zikiwa Kombe la Shirikisho Afrika.
Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2007 ilipoanza Kombe la Mapinduzi kuchezwa kwa kushirikisha timu kutoka nje ya Zanzibar, klabu mbili pekee kutoka visiwani humo zimebeba ubingwa ambazo ni Miembeni (2009) na Mlandege iliyobeba mara mbili 2023 na 2024.
