Dodoma. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, ametaka kutolewa kwa mafunzo maalumu ya ulinzi wa data kwa watumishi wa Serikali na wanafunzi, hususani wa vyuo.
Maagizo yametolewa kwa taasisi za elimu ya juu ikiwemo vyuo vikuu, na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) zikitakiwa kushirikiana na Wizara ya elimu ili kutoa maelekezo ya matumizi ya akili unde kwa njia sahihi katika tafiti, uchakataji wa data na utawala bora kwa njia salama.
Profesa Nombo ameyasema haya leo Jumatano, Januari, 14 2025 wakati akizungumza na wadau wa elimu nchini wakiwemo wakuu wa vyuo kwenye warsha iliyokuwa na lengo la kusambaza mkakati wa Taifa wa elimu kidijitali 2030 na mwongozo wa utekelezaji wake iliyofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye warsha hiyo Profesa Nombo amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwajengea uwezo wa kutambua hatari ikiwemo wizi wa taarifa wakati wa utumiaji wa teknolojia kwenye ujifunzaji, ufundishaji na utekelezaji wa majukumu ya kikazi.
“Wakati tunaendelea na matumizi ya kidijitali ni lazima kuweka sera madhubuti kwa ajili ulinzi wa taarifa na data ili kuepusha wizi wa taarifa za watu binafsi au taasisi,”amesema Profesa Nombo.
Profesa Nombo ameonya kuwa matumizi yasiyo salama ya teknolojia ya akili unde yanaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo wizi wa taarifa binafsi na za taasisi, ukiukwaji wa faragha na matumizi mabaya ya data.
Amezishauri pia mamlaka hizo kuweka mikakati ya kuhakikisha elimu ya kidijitali inatolewa kwa ufanisi katika maeneo ya vijijini ili kuwafikia wanafunzi wanaotoka kwenye mazingira magumu, ikiwemo ufungwaji wa mkongo wa Taifa kwenye kila wilaya ili kurahisisha upatikanaji wa intaneti.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladslaus Mnyore, ameshauri kuangiliwa upya kwa marufuku ya matumizi ya simu na vifaa vya kieletroniki kwa wanafunzi wawapo shuleni.
“Ikiwezekana wanafunzi waruhusiwe kutumia simu kwa kuwekewa utaratibu mzuri na kupewa maelekezo yatakayosaidia matumizi salama ya vifaa hivyo, kwani huvitumia wakiwa nyumbani lakini wakija shuleni huzuliwa jambo linaloenda kinyume na sera ya kidijitali”amesema Profesa Mnyore.