Serikali yawaalika wadau kushiriki kuimarisha sekta ya elimu

Pwani. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewataka wadau mbalimbali wa elimu wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kushirikiana na Serikali kwa ajili kuendelea kuboresha maeneo mbalimbali katika sekta ya elimu.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Januari 14, 2026 wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa matundu 12 ya vyoo kwa wanafunzi wa kike, matundu mawili ya walimu, eneo la kunawia mikono, chumba maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, chumba cha kujisitiri kwa wasichana, pamoja na eneo la kuchomea taka, hususan taulo za kike zilizotumika.

Akizungumza kwa niamba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo,  Shaibu Ndemanga amesema kuwa mradi huo ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuboresha elimu.

“Serikali inaendelea kuwakaribisha wadau kama Taasisi ya Flaviana Matata kushirikiana nasi katika kutatua changamoto za msingi shuleni. Amesema mradi huo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia, hasa kwa watoto wa kike,” amesema Ndemanga.

Taasisi ya Flaviana Matata imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu na afya kwa kuzindua na kukabidhi rasmi mradi wa vyoo na huduma za maji safi na salama katika Shule ya Sekondari Kiwangwa.

Lengo kubwa la taasisi hiyo ni kuboresha mazingira ya shule na kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto wa kike katika safari yao ya kielimu.

Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Flaviana Matata, Flaviana Matata amesema taasisi hiyo ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha watoto wa kike wanapata mazingira salama na rafiki yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao.

Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Safar Global Foundation ambao wamefadhili ujenzi wa vyoo hivi. Asante kwa kuamini kile tunachokifanya, na kwa kujitolea kwenu kuhakikisha tunafanikisha hili. Siku ya leo tunavyokabidhi hivi vyoo ni nafasi inayotoa heshima, usalama, na msingi wa elimu bora hasa kwa wasichana.”

“Pia, tulijenga vyoo kwa ajili ya walimu kwa sababu tunapowaunga mkono walimu, tunaimarisha mazingira yote ya kujifunzia. Hivyo leo, kwa kweli tunasaidia pande zote mbili: wanafunzi na hii inawakilisha heshima, ushirikiano, na dhamira ya pamoja kwa elimu na heshima.” amesema.

Ameongeza kuwa, “Tunatambua kuwa changamoto za usafi wa mazingira, hususan ukosefu wa vyoo rafiki kwa wasichana, zimekuwa kikwazo kwa elimu yao. Mradi huu ni sehemu ya mchango wetu katika kuhakikisha hakuna mtoto wa kike anayekosa elimu kwa sababu ya mazingira duni.”

Waanzilishi wa Safar Global Foundation, Shabnam  Safarzadeh na Shay Safarzadeh wamesema taasisi hiyo imefurahi kushirikiana na Taasisi ya Flaviana Matata katika mradi unaogusa moja kwa moja maisha ya watoto wa kike.

“Tunaamini uwekezaji katika afya, usafi wa mazingira na elimu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa jamii. Tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuleta mabadiliko chanya,” amesema Safarzadeh.      

Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa serikali, walimu, wazazi, wanafunzi pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Mradi huo unaotekelezwa kwenye Shule ya Sekondari ya Kiwanga mkoani Pwani chini ya Taasisi ya Flaviana Matata kwa ufadhili wa Safar Global Foundation unatarajiwa kuwanufaisha wanafunzi 930 kila mwaka.

Aidha wanafunzi hao watapata huduma bora za vyoo na maji safi na salama, hali inayotarajiwa kuboresha afya, usafi wa mazingira, mahudhurio ya wanafunzi shuleni na hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu.