Dar es Salaam. Wananchi wanaotumia usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi kwa Barabara ya Kimara, wameeleza adha wanazopitia baada ya mabasi ya Kampuni ya Mofat kusitisha kutoa huduma katika barabara hiyo kwa wiki mbili sasa sawa na siku 14.
Mwananchi wiki hii imetembelea vituo mbalimbali vya mabasi kuanzia Kariakoo Gerezani, Kivukoni na Kimara na kushuhudia kutokuwepo kwa mabasi hayo huku yaliyokuwa yakifanya kazi ni yale yanayomilikiwa na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) japo pia yalionekana kuchelewa kufika vituoni licha ya kuwa abiria nao hawakuwa wengi.
Akizungumza jana Jumanne Januari 13, 2026, kuhusiana na hatua hiyo, baada Mwananchi kumtafuta, Ofisa Mkuu wa Uendeshaji wa Kampuni ya Mofat, Mabrouk Masasi, ametaja sababu za kusitisha kutoa huduma ni kutokana na mkataba wao kuisha ambao ilikuwa ni kutoa huduma ndani ya miezi mitatu (yaani Oktoba 1 Desemba 31, 2025).
“Ni kweli tumesitisha kutoa huduma tangu Desemba 31, 2025 baada ya mkataba wetu kuisha, lakini kama tutahitajika tena tupo tayari kuwahudumia wananchi kwa kuwa mabasi tunayo ya kutosha kwa kuwa mpaka sasa tumeshaleta magari 200 na yaliyoingizwa barabarani ni 40 tu,” amesema Mabrouk.
Kusitisitishwa kwa mabasi hayo pia kumethibitishwa na serikali kupitia Msemaji Mkuu wake, Gerson Msigwa, alipozungumza leo Jumatano 15, 2026 na Mwananchi.
Hata hivyo, Msigwa amesema baada ya wao nao kugundua uwepo wa changamoto ya usafiri, imeamuliwa Mofat waongezwe mkataba mwingine wa mwezi mmoja.
Akieleza sababu ya kufanya uamuzi huo, Msigwa amesema ukiacha malalamiko ya wananchi kuhitaji mabasi mapya na unafuu wa usafiri, lakini pia yale 49 yaliletwa na Kampuni ya Udart, bado yapo katika mchakato wa kuweza kuingizwa barabarani ambao hauwezi kukamilika leo au kesho.
Baadhi ya mabasi ya mwendokasi yanayotoa huduma Kimara yalivyo ndani
“Serikali tumeona kiu ya wananchi ni mabasi mapya, hivyo imeamuliwa wakati yale mapya ya Udart yakisubiriwa kumaliza mchakato wake wa kuingizwa barabarani, Mofat waendelee kutoa huduma ndani ya mwezi mmoja,” amesema Msigwa.
Ikumbukwe mwaka jana, Serikali iliruhusu mabasi ya Mofat kuhudumia barabara ya Kimara ambayo kimkataba yameletwa kwa ajili ya kutoa huduma katika barabara ya Mbagala.
Uamuzi huo ulitangazwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Oktoba 2, 2025, alipofanya ziara kukagua hali ya utoaji huduma ya usafiri wa mabasi hayo Kivukoni hadi Kimara jijini Dar es Salaam.
Majaliwa alisema Serikali iliamua kuingiza mabasi 60 mapya kwenye barabara hiyo iliyokuwa na mabasi 30 yanayofanya kazi ili kukabiliana na upungufu uliokuwepo.
Kwa upande wao wananchi wakitoa maoni kwa nyakati tofauti kuhusiana na hatua hiyo, Gumbo Hemed, mkazi wa Kimara, amesema haikuwa sahihi kwa huduma hizo kusitishwa kimyakimya huku akipongeza hatua ya Serikali kuwaongezea muda Mofat.
Badala yake Hemed amesema Serikali ilipaswa kutangaza maamuzi yake ya kuyaruhusu mabasi hayo ya Mofat kufanya kazi, hata usitishwaji wake walipasa kutaarifiwa na sio kuondolewa kimyakimya kama ilivyofanya.
“Kiukweli serikali haijatutendea haki, ukizingatia wengine tulishaamua kuacha magari yetu nyumbani na kupanda mabasi hayo, sasa leo kuyaondoa kimyakimya barabarani bila kutupa taarifa sio sawa na tulijua yatafanya kazi hadi ya Udart yatakapoweza kuingia barabarani,” amesema.
Naye Farida Joel, mkazi wa Kigamboni anayefanya shughuli zake Mbezi, amesema mabasi hayo yaliwahishwa kutolewa barabarani hata kama hayo ya Udart yameshafika.
Farida amesema hii ni kutokana na uzoefu kwamba mabasi hayo yakiingia nchini mchakato wake huchukua muda mrefu hadi kuingizwa barabarani hivyo changamoto za usafri huo ilikuwa lazima irudi kama zamani.
Edger Mbiro amesema alitarajia sasa hivi Udart ndio wangejirekebisha ili kurudisha imani kwa wananchi, lakini ni kama wanafanya kazi kimazoea na kutaka serikali iliangalie hilo kuepuka kuja kupata hasara baadaye baada ya kuja kwa mwekezaji mwingine.
Mbiro amesema hata mabasi yaliyoko kimuonekano yamechoka, hata hujui lipi limetengenezwa lipi bovu.
Fideline Lymo mkazi wa Kibamba, amesema uchache huo wa abiria ni kutokana na historia waliyonayo kuhusu tabu za usafiri huo hivyo mtu anaona ni bora apande zake bajaji au bodaboda ili awahi kwenye mihangaiko yake kwa kuwa anawajua waendeshaji wa mabasi hayo japo inawaongezea gharama za maisha,”amesema Fideline.
Kwa upande wao wachumi, akiwemo Profesa Haji Semboja, amesema pamoja na mabasi kuletwa lakini bado kuna changamoto ya mifumo katika uendeshaji.
“Kuendesha huo mradi kunahitaji utaalamu wa juu, inaitwa mwendokasi lakini si mwendokasi,” amesema.
Amesema kama barabara zake zote zitamalizika, zikaondolewa daladala na bodaboda katika njia hizo na kuwepo usafiri wa uhakika, tutapiga hatua kubwa zaidi.
Mchumi mwingine, Oscar Mkude kusuasua kwa mradi moja ya athari yake ni kuchelewa kurudisha gharama za uendeshaji.
“Mradi unatakiwa ujiendeshe, unaposuasua ni hasara, swali la kujiuliza tangu uanze hadi sasa bado tuko kwenye kujifunza,” amehoji Mkude.
Amesema huo ndiyo mradi ambao shida sio wateja bali ni mtoa huduma kushindwa kuwahudumia hao wateja.
“Katika hali kama hiyo ingekuwa ni sekta binafsi asingekubali, tunapitia hali hii sababu ni mradi wa Serikali na ilii kutoka huko, kwanini asitafutwe mtoa huduma mwenye uzoefu,” amehoji.
