Video: Marekani Yatingisha Iran, Trump Aonya Kabla ya Mazungumzo



Rais wa Marekani, Donald Trump amerudia maonyo yake ya kutaka kuingilia masuala ya Iran, akisema anaweza kuchukua hatua kabla ya kukutana na maafisa wa Iran kwa kuwa nchi hiyo imevuka mstari mwekundu.

Trump hajasema ni hatua gani anazokusudia kuchukua na alipoulizwa jana Jumatatu afafanue Iran imevuka mstari gani mwekundu, alisema:

“Ndiyo, inaonekana imevuka mstari mwekundu.Tunaangalia hili kwa umakini mkubwa. Jeshi pia linaangalia hili kwa umakini sana. Tunafikiria hatua kadhaa. Tutafanya uamuzi.”

Kundi la waangalizi lenye makao yake nchini Marekani, linasema zaidi ya watu 500 wamefariki dunia katika maandamano ya Iran tangu Desemba 28 mwaka jana.

RaisTrump tayari ameonya kwamba Marekani itaingilia kati kuwalinda waandamanaji nchini Iran ikiwa watazidi kuuawa.

Video imeibuka ya chumba cha kuhifadhia maiti cha muda kilichowekwa nje kidogo ya mji mkuu wa Iran, Tehran. Wairani wengi wamekwenda huko kuwatafuta wapendwa wao.

Kwa mujibu wa televisheni rasmi ya Iran, watu walionekana wakiwa wamebeba majeneza yenye miili ya askari wa vikosi vya usalama na raia katika majimbo 10 kwa ajili ya mazishi.

Wataalam na mashuhuda wanasema maandamano ya kupinga serikali nchini Iran yamekuwa makubwa kiasi kwamba hayajawahi kuonekana hapo awali katika historia ya miaka 47 tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.