Wasomi, wajasiriamali kujadili ukuaji wa uchumi unaojumuisha watu wote

Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Shule ya Biashara (UDBS) limeandaa kongamano la Kimataifa la Ujasiriamali wa Afrika na Maendeleo ya Biashara Ndogo (ICAESB) la kujadili kwa namna gani biashara za Afrika zinaweza kuwa chachu ya ukuaji jumuishi na endelevu.

Kongamano hilo 20 litakalofanyika Januari 15 na 16, 2025 ni jukwaa litakalowakutanisha watafiti, watunga sera, wajasiriamali na viongozi wa sekta binafsi kutoka ndani na nje ya Afrika wakiwasilisha ujuzi, uzoefu na tafiti zinazolenga kuinua biashara ndogo na za kati (SMEs) pamoja na kukuza ujasiriamali barani Afrika.

Akizungumzia kongamano hilo leo Januari 14, 2025 Mkuu wa UDBS, Profesa Omary Mbura amesema mkusanyiko huo ni fursa ya kipekee kwa washiriki kubadilishana mawazo na kufanya mtandao wa ushirikiano wa kimataifa uliolenga kuchochea ukuaji wa uchumi unaojumuisha watu wote.

Amesema kongamano hilo pia litatoa nafasi ya kujadili changamoto zilizopo katika mazingira ya biashara ndogo, pamoja na suluhisho za kisayansi na mbinu za kisasa za kibiashara.

“Kama taasisi ya biashara na elimu, tuna dhamira ya kuchangia katika utungaji wa sera kwa kuwasilisha mapendekezo muhimu kwa taasisi husika za Serikali za kitaifa na kikanda,” amesema.

Kwenye kongamano hilo linalobebwa na kaulimbiu ‘Kubadilisha biashara kwa maendeleo endelevu’, zaidi ya mada 60 za tafiti zitawasilishwa zikilenga kuchunguza mbinu bora za kuunganisha ujasiriamali na ukuaji wa kiuchumi, hasa katika mazingira ya soko la kimataifa, wakati ambao SMEs zinazidi kuwa nguzo ya uchumi wa nchi nyingi.

Wachumi wameeleza kuwa ICAESB ni jukwaa muhimu katika kujenga msingi wa ukuaji wa uchumi unaojumuisha watu wengi barani Afrika, hususan kupitia biashara ndogo na za kati (SMEs).

Akizungumzia na Mwananchi, Dk Godwin Mjema anasema kongamano hilo linakuja wakati mwafaka ambapo nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania, zinatafuta njia mbadala za kukuza uchumi unaotegemea zaidi sekta binafsi.

Amesema SMEs ndizo mhimili wa ajira na uzalishaji, lakini bado zinakabiliwa na changamoto za mitaji, masoko na teknolojia.

“Majukwaa kama ICAESB husaidia kuunganisha nadharia na vitendo kwa kuwakutanisha watafiti, watunga sera na wajasiriamali. Hii ni fursa ya kupata suluhisho za kisayansi zinazoweza kutafsiriwa moja kwa moja kuwa sera rafiki kwa biashara ndogo,” amesema Dk Mjema ambaye ni mtaalamu wa uchumi.

Kwa upande wake, mtaalamu wa biashara na uwekezaji, Anna Mvungi amesema tafiti nyingi zimeonyesha kuwa biashara ndogo zinapopewa mazingira bora ya sera, miundombinu na maarifa, huongeza tija na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa.

“Kaulimbiu ya kubadilisha biashara kwa maendeleo endelevu inaendana na ajenda ya sasa ya kiuchumi, ambayo haitazami faida pekee, bali pia athari za kijamii na kimazingira,” amebainisha.