ADAKWA KWA WIZI WA CHUPI ZA JIRANI YAKE

……..

GEITA 

“Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Filauni” ndivyo wasemavyo wahenga.

Msemo huo umechagizwa na tukio la Felista Tablei, mkazi wa mtaa wa Mkoani Kata ya Kalangalala Manispaa ya Geita baada ya kutuhumiwa kuiba nguo za ndani za jirani yake.

Hatua hiyo imetokana na ugomvi wa mtuhumiwa na jirani yake aliyefahamika kwa jina la Odetha Dickson, ambaye alimtuhumu kumrubuni binti yake wa kazi na kuhamia kwake licha ya gharama kubwa alizotumia kumpata.

Kutokana na hali hiyo, Felista akalazimika kumuibia jirani yake nguo za ndani na kuchana shuka hatua iliyosababisha kufikishwa kwenye Ofisi ya serikali ya mtaa wa mkoani ili kujibu tuhuma zinazomkabili. 

“Tumezungumza na Felista kutaka kufahamu undani wa tukio hilo ambapo amekiri kuchukua nguo ya ndani moja na dela la jirani yake kutokana na ugomvi wao uliochangiwa na dada wa kazi aliyekuwa akifanya kazi kwake kabla ya kuhamia kwa jirani yake”.

Kwa upande wake, Odetha (aliyeibiwa) amekiri kuwa na ugomvi na jirani yake huyo, na kudai kuwa kitendo alichofanyiwa siyo cha kiungwana na kwamba kina nia ovyo huku akiomba kurejeshewa nguo zake za ndani.

Kutokana na maelezo yaliyotolewa na pande zote mbili, Ofisi ya mtaa chini ya Mwenyekiti wake, Salvatory Daniel na baada ya mtuhumiwa kukiri kosa kwa kunywa chake mwenyewe, imefikia uamuzi kumwadhibu kulipa faini ya Shilingi 75,000 ili kulipia gharama za nguo hizo.

Chanzo: Radio tadio