Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema atatumia muhula wake wa pili madarakani kukarabati, kujenga upya na kulihuisha Taifa kufuatia vurugu zilizojitokeza wakati ya baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Rais Samia amesema hayo leo Alhamisi Januari 15, 2026 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya kufungua mwaka pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.
Katika hotuba yake, Rais Samia amezungumzia nyakati ngumu ambazo Tanzania imezipitia tangu uchaguzi ulipofanyika huku akitoa wito kwa mabalozi hao kushirikiana na Serikali sambamba na kuheshimu uhuru wa nchi.
Siku ya uchaguzi mkuu, kulizuka maandamano yaliyotawaliwa na vurugu, baadhi ya vijana waliolenga kuzuia uchaguzi huo, walikuwa wakichoma mali za umma na binafsi pamoja na kuharibu miundombinu hususani vituo vya mabasi yaendayo haraka (BRT).
Rais Samia Suluhu Hassan azungumza na Mabalozi katika sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) Ikulu ya Chamwino -Dodoma
Katika kukabiliana na watu hao, vyombo vya dola vilitumia nguvu kuwadhibiti waandamanaji hao kwa kuwapiga risasi.
Baadhi yao walipoteza maisha katika maandamano hayo huku wengine wakijeruhiwa.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Samia amewaeleza mabalozi ili kuliponya Taifa, amesema amechukua hatua kadhaa, ikiwamo kuunda Wizara ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais ili kuijengea taasisi nguvu ya kizazi kijacho.
Pia, amesema ametoa msamaha kwa vijana 1,787 waliokamatwa kwa kuhusika na vurugu za siku ya uchaguzi.
Hatua nyingine alizozichukua, amesema ni kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na ahadi ya kuunda Tume ya Maridhiano ikiwa ni hatua ya kwenda kwenye mchakato wa kutengeneza Katiba mpya.
Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, pamoja na Wawakilishi wa Heshima wakiwa kwenye sherehe ya mwaka mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe 15 Januari, 2026.
“Serikali yangu imejipanga kutumia kipindi hiki cha pili kukarabati, kujenga upya na kulihuisha Taifa letu.
“Kwa Watanzania wenzangu, ghasia tulizozishuhudia sivyo tulivyo, sivyo kabisa. Kwa wadau wetu wa kimataifa, tunatambua ustahimilivu wa kidiplomasia. Tunaamini kwamba njia yetu itajengwa kwa msingi wa haki, majadiliano na heshima mpya katika mchakato wa kidemokrasia,” amesema.
Rais Samia amesema Tanzania ni moja ya nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi, ikiwa na ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) la asilimia sita huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwa asilimia 3.3.
Kadhalika, amesema deni la Taifa limeendelea kuwa himilivu, uwiano wa deni katika GDP ukiwa ni asilimia 40.2, chini ya ukomo wa asilimia 55 kwa nchi za uchumi wa chini.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amewashukuru washirika wa kimataifa walioonesha mshikamano na Tanzania wakati wa uchaguzi, hata hivyo amewataka wasioshiriki katika mtazamo wa Serikali kuheshimu uhuru wa nchi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, pamoja na Wawakilishi wa Heshima katika sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza Ikulu ya Chamwino, Dodoma Januari 15, 2026.
“Kwa wale walioonesha mshikamano na kutuma meseji za pongezi, tunawashukuru sana. Kwa wale ambao hawakufanya hivyo, tumechukua mrejesho wenu pia.
“Ninawaomba marafiki wetu kutoa ushirikiano katika mabadiliko yetu na kwa wale ambao hawatashiriki mtazamo wetu, ninaomba angalau uhuru wetu kama nchi,” amesema mkuu huyo wa nchi katika hotuba yake.
Rais Samia amesisitiza kwamba sauti za Watanzania zimesikika kupitia sanduku la kura na sauti hizo lazima ziheshimiwe.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Thabit Kombo akizungumza kwenye sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe Januari 15, 2026.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema mwaka 2025, Tanzania ilikabiliwa na vurugu wakati wa uchaguzi ambazo hazijawahi kutokea tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.
Amesema vurugu hizo zimekuwa na athari kubwa kwa Tanzania katika msimamo wake na taswira yake duniani.
“Hapa nyumbani tulishuhudia ghasia na mashambulizi na mali za umma na binafsi zote zikiharibiwa ikiwamo watu kupoteza maisha. Huko nje tulishuhudia kuzuiwa kwa fedha na kukosekana uhakika wa kiuchumi,
“Sera yetu ya Mambo ya Nje ilipitia majaribu kwa mara ya kwanza katika historia tangu Uhuru, miaka 64 iliyopita,” amesema Balozi Kombo.
Amesema baada ya kuteuliwa, alipokea jumbe nyingi za kufariji kutoka kwa marafiki na washirika, baadhi walionesha kuguswa na kilichotokea wakati wengine wakiuliza, nini kimetokea Tanzania.
Kiongozi wa mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, Ahamada El Badaoui Mohamed, ambaye ni Balozi wa Comoro nchini Tanzania, amesema kwa niaba ya mabalozi wengine, anampongeza kwa kushinda uchaguzi kwa awamu ya pili kuendelea kuwa na dhamira ya kushirikiana na mataifa mengine.
Balozi El Badaoui amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee katika Kanda ya Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa jumla, kwani inatambulika kama nchi ya amani.
Amidi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Comoro nchini Tanzania Ahmada El Badaoui Mohamed Fakih, akizungumza kwenye sherehe ya Mwaka Mpya kwa Mabalozi (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika kwa mara ya kwanza, Ikulu ya Chamwino, Dodoma tarehe Januari 15 , 2026.
“Katika eneo la biashara, ni wazi kwamba Tanzania inaendelea kuonesha dhamira na uwezo wake katika kipindi ambacho dunia inapitia wakati mgumu na kwa kweli tumeona jitihada zako katika kutunza amani na utulivu,” amesema.
Amesema walifuatilia yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi na wakaona namna Serikali ilivyoweza kulisimamia suala hilo.
Hata hivyo, amesema wamefurahishwa alivyounda Tume ili kuzuia matukio hayo yasijirudie tena siku zijazo.