Aliyeshtakiwa kutapeli kwa jina la Mchungaji Kulola amshinda DPP

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Tanga, imetupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Tanga, iliyomuachia huru Jane Samwel aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la kujipatia gari kwa njia ya udanganyifu.

Mahakama hiyo katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Messe Chaba, imekubaliana na hukumu ya Mahakama ya Wilaya kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka yoyote, kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria katika kesi za jinai.
Mahakama hiyo katika hukumu yake ya Desemba 31, 2025 imeitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na sababu za rufaa za DPP kutokuwa na mashiko kisheria.

Jaji Chaba amesema kuwa baada ya kuchunguza kwa makini rekodi ya mahakama ya chini, sababu za rufaa, na hoja za maandishi zilizowasilishwa na pande zote mbili, sababu zote nane za rufaa kimsingi zinahusu swali moja kuu, yaani, kama upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake dhidi ya mjibu rufaa.

Amesema ingawa madai ya udanganyifu yalikuwa na uzito lakini upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi muhimu hasa ujumbe wa maandishi uliodaiwa kuwa msingi wa udanganyifu huo.

Amesema kuwa Mahakama bila ujumbe huo au uthibitisho kutoka kampuni za simu au Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) haiwezekani kuthibitisha kuwa mjibu rufaa ndiye aliyekuwa chanzo cha udanganyifu.

Jaji Chaba amesisitiza kuwa katika kesi za jinai mzigo wa kuthibitisha kosa unabaki upande wa mashtaka na endapo kuna shaka yoyote, mshtakiwa hunufaika na shaka hiyo.

Amefafanua kuwa upande wa mashtaka ungeweza kupata ushahidi kutoka kwa mtoa huduma za simu za mkononi au TCRA ili kuthibitisha umiliki wa namba zilizotumika na kubaini kama zilitumiwa na mjibu rufaa kufanya madai ya uongo.

Jaji Chana amesisitiza zaidi kuwa ushahidi kama huo ungemuhusisha moja kwa moja mjibu rufaa na uhalifu unaodaiwa, kwa kukosekana kwa ushahidi huu muhimu, madai ya kupata mali kwa uongo bado hayajathibitishwa.

“Kwa sababu zilizo hapo juu, naona na kuamua kwamba, Mahakama ya awali ilichambua ushahidi ulio mbele yake kwa usahihi na ipasavyo, na kusababisha mjibu mashtaka kuachiwa huru, kwa hivyo rufaa hii haina msingi na imetupiliwa mbali kabisa,”amehitimisha.

Pia Jaji Chaba ameamuru gari hilo aina ya Noah liendelee kubaki kwake Jane akieleza kuwa amesajiliwa kisheria.

 

Kesi ya msingi

Katika kesi ya msingi, kesi ya jinai 61/2018, Jane alidaiwa kutenda kosa la kujipatia mali kwa njia za udanganyifu kinyume na kifungu cha 302 cha Kanuni ya Adhabu.

Alidaiwa kuwa alijipatia ambapo alidaiwa kupata gari aina ya Noah lililokuwa na namba za usajili T 232 CML, lenye thamani ya Sh11.3 milioni kutoka kwa Luice Makame.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande uliwaita mashahidi wawili ambao ni Luice na Lucy Charles ambao ni mume na mke.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka, Jane alikuwa rafiki wa karibu wa shahidi wa pili (Lucy) na kupitia urafiki huo, Jane aliwatambulisha wanandoa hao kwenye mtandao aliodai ni wa wachungaji maarufu akiwemo marehemu Mchungaji Kulola.

Kwa tarehe tofauti kuanzia Julai 2011, Lucy alipokea ujumbe kutoka kwa namba kadhaa za simu za mkononi, ambazo zilidaiwa kuwa za Mchungaji Kulola na mke wake (Magreth Kulola).

Katika ujumbe huo, wanandoa hao waliombwa mara kwa mara kutuma fedha kwa ajili ya sadaka, ankara za maji na umeme pamoja na kusaidia shughuli mbalimbali za kidini.

Baadaye Jane alidai kusafiri kwenda Uganda kuhudhuria semina na kusaidia watoto watatu ambao walikuwa hawatembei na kuwa wazazi wa watoto hao walimzawadia gari hilo aina ya Noah kama Ishara ya shukurani.

Kutokana na ugumu wa kusafirisha gari hilo kutoka Uganda, iliamuliwa liuzwe kwa bei ya Sh12 milioni fedha ambazo zilidaiwa kutumwa kwa Mchungaji Kulola jijini Mwanza.

Wanandoa hao baadaye walidai kupokea ujumbe kuwa fedha hizo ziliibwa na kuwa endapo zisingerejeshwa Mchungaji Kulola angepata adhabu ya kuwa mlemavu.

Ujumbe mwingine uliofuata, ukiwaomba mashahidi hao wawili kusaidia kukusanya kiasi hicho, ambapo waliamua kubeba mzigo wa kununua gari hilo na kumkabidhi Jane fedha hizo, baada ya kukopa kutoka kwa mama mkwe wa Luice, fedha ambazo zililipwa kupitia akaunti namba ya Lucy.

Kwa mujibu wa ushahidi wake Lucy, Julai 27, 2013 alitoa pesa hizo na kuweka kwenye akaunti ya CRDB namba  inayomilikiwa na Elibariki Mushi wa Dar es Salaam kwa maelekezo toka kwa ujumbe mfupi uliodaiwa umetoka kwa mke wa Kulola (Magreth Kulola).

Uhusiano wa ndoa kati ya mashahidi hao ulizorota ambapo Luice baadaye alianza kutilia shaka kama namba hizo za simu ni kweli za Kulola, baadaye walibaini kuwa Jane ni tapeli hivyo wakaripoti Polisi.

Kwa upande wake Luice kwa mujibu wa ushahidi wake , kufuatia kifo cha Mchungaji Kulola, ripoti za vyombo vya habari zilimtambua Elizabeth Kulola kama mke wa marehemu, jambo ambalo lilimshangaza kwani Jane hapo awali aliwakilisha kwamba, mke wa marehemu alikuwa anaitwa Magreth.

Katika hali hiyo, Jane alikamatwa na kushtakiwa, na gari husika lilikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.

Utetezi wa Jane

Katika utetezi wake, Jane alikana madai hayo akieleza kuwa hakuwahi kujifanya Mchungaji Kulola wala kumtumia ujumbe wowote wa udanganyifu mtu na kudai kuwa gari hilo aina ya Noah alipewa kama zawadi.

Alidai kuwa kutokana na urafiki wake wa karibu na Lucy, ambapo pia alikuwa msimamizi wa sherehe ya harusi ya mashahidi hao, ambapo katika shughuli hiyo alitambulishwa kwa mama wa Lucy na kudai mama huyo alimpa gari hilo kama zawadi baada ya kumsaidia binti yake katika harusi.

Mahakama ya wilaya baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote katika hukumu yake Agosti 18,2021, ilimwachilia huru Jane baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha shtaka lililokuwa linamkabili, kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, yaani bila kuacha shaka yoyote ya msingi.

DPP hakukubaliana na hukumu hiyo, hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu, kuipinga hukumu hiyo ya Mahakama ya Wilaya huku akitoa sababu nane.

Rufaa ya DPP

Katika rufaa hiyo ya jinai namba namba 535566/2023, DPP aliainisha sababu nane za kupinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ikiwemo Hakimu alikosea kisheria kushindwa kutathmini ushahidi wa upande wa mashtaka.

Sababu nyingine alidai kuwa Hakimu alishindwa kugundua kwamba Jane alitoa uwakilishi wa uongo kwa shahidi wa kwanza na wa pili na matokeo yake alipata gari kwa njia za udanganyifu.

Nyingine ni Hakimu kufanya makosa kisheria na kumwachia huru mshtakiwa kwa madai kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha kwamba gari hilo ni mali ya Luice, kwa madai kuwa usajili wa kadi ulipatikana kwa njia ya udanganyifu.

Sababu nyingine ni Mahakama ya awali kufanya makosa kisheria kuagiza kurejeshwa kwa gari hilo kwa Jane kwani hakuwa na haki ya kulimiliki.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Wakili wa Serikali, alidai kuwa Hakimu alishindwa kugundua kuwa Jane alitoa maelezo ya uongo kwa shahidi wa kwanza na wa pili na kuwa alijificha utambulisho wake kupitia ujumbe mfupi wa simu na kujifanya Mchungaji Kulola.

Pia alidai kuwa mashahidi hao walitenda kwa imani na huzuni ya kidini na kutapeliwa kutoa Sh12 milioni kumwokoa Mchungaji.

Aliieleza mahakama kuwa kwenye ukurasa wa 107 wa kumbukumbu za shauri hilo, Jane alikiri kutomjua Mchungaji Kulola hivyo huo ni uthibitisho kuwa alitoa maelezo ya uongo ili kupata gari hilo.

Alidai kuwa Hakimu alikosea kwa kutegemea tu kadi ya usajili ili kubaini umiliki bila kuzingatia kwamba, usajili ulipatikana kwa udanganyifu na shahidi wa kwanza alithibitisha pesa hizo zilikuwa mkopo kutoka kwenye pensheni ya kustaafu ya mama mkwe wake (Vumpoa Mzava).