Bobi Wine apiga kura, wafuasi wake wamsindikiza kituoni

Uganda. Mgombea urais wa upinzani kupitia Chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine amepiga kura eneo la Free Square, Magere katika Wilaya ya Wakiso nchini Uganda.

Bobi Wine amewasili kituo cha kupigia kura leo Alhamisi Januari 15, 2026, akiwa ameambatana na mkewe, Barbie Kyagulanyi ambapo wote kwa pamoja walipiga kura katika kituo hicho.

Pia, umati wa wafuasi wake walimfuata kwa nyuma wakati akielekea kituo cha kupiga kura na kushikana mikono ili kumuwekea ulinzi, huku maofisa wa polisi wakimsindikiza wakiwa wameimarisha usalama wake.

Maafisa wa usalama wakiwa macho wakati kiongozi wa Upinzani na mgombeaji urais wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu (Bobi Wine), alipowasili kupiga kura mnamo Januari 15, 2026 katika Freedom Square huko Magere, Wilaya ya Wakiso. PICHA na ABUBAKER LUBOWA

Tofauti na alivyozoeleka kuonekana akiwa amevalia mavazi yake pamoja na kofia ngumu na koti la kuzuia risasi kifuani, leo alikuwa amevalia Kaunda suti pekee yenye rangi ya bluu.

Hata hivyo Bobi Wine, ametoa kauli baada ya Rais Yoweri Museveni kudai kuwa baadhi ya maofisa wa Tume ya Uchaguzi (EC) huenda walihujumu kimakusudi matumizi ya mashine za uthibitishaji wa wapiga kura kwa njia ya bayometriki.

Amekosoa kukwama matumizi ya mashine za bayometriki, akisema kuwa zimeshindwa kufanya kazi licha ya serikali kutumia mabilioni ya fedha.

“Walipoteza mabilioni ya fedha za walipa kodi na kununua mashine hizi ili kuzitumia kusaidia udanganyifu wa uchaguzi. Hata hazifanyi kazi. Tunaendelea kuwahamasisha Waganda waendelee kulinda kura zao,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Tunajua vyombo vya usalama vinataka kujaribu kuiba ushindi wetu. Kwa hiyo, iwapo vyombo vya usalama na EC vitajaribu kupindua uamuzi wa Waganda, raia wana haki ya kupinga kwa njia isiyo na silaha na isiyo ya vurugu.”

Amezishutumu mamlaka kwa kutumia teknolojia isiyofanya kazi ipasavyo na akawahimiza wananchi kulinda kura zao.

Kiongozi wa upinzani na mgombea urais wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu akiongozana na mkewe Barbie Kyagulanyi wakiwasili katika viwanja vya Freedom Square eneo la Magere Wilaya ya Wakiso ambako walipiga kura Januari 15, 2026. PICHA na ABUBAKER LUBOWA

Pia, alilaani kukamatwa kwa Makamu wa Rais wa Chama cha National Unity Platform (NUP) kwa Kanda ya Magharibi, Jacklyn Jolly Tukamushaba, ambaye amesema amesafirishwa na kupelekwa kusikojulikana.

Awali, Museveni, mwenye umri wa miaka 81, amepiga kura saa saa 5 asubuhi na amesema kuwa baadhi ya maofisa wa EC huenda walichelewesha kimakusudi kupakia taarifa binafsi za wafanyakazi zinazohitajika ili mashine hizo zifanye kazi hivyo ameagiza uchunguzi kufanyika.