Diwani kuwasaka watoto wenye ulemavu waliofichwa ndani

Moshi. Ikiwa zimepita siku tatu tangu kufunguliwa kwa shule nchini, diwani wa kata ya Rau, Manispaa ya Moshi, Stallone Malinda, amesema ofisi yake itaanzisha msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini watoto wenye ulemavu waliofichwa majumbani na wazazi wao, hali inayowanyima fursa ya kuandikishwa shule.

Amesema wapo baadhi ya wazazi ambao wamekuwa na tabia ya kuwaficha watoto ndani hali ambayo amesema ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu sawa na watoto wengine.

Diwani Malinda ameyasema hayo leo, Januari 15, 2025 wakati alipotembelea Shule ya Msingi Rau yenye wanafunzi 643, iliyopo katika kata hiyo, kujionea hali ya mwitikio wa wanafunzi kuripoti shuleni baada ya shule kufunguliwa Januari 13, 2026.

Aidha, amesema kuwa Serikali na wadau wa elimu wameweka mazingira rafiki kwa ajili ya watoto hao hivyo hakuna sababu ya mzazi kumzuia mtoto kwenda shule, akisisitiza kuwa hatua zitachukuliwa kwa wazazi watakaobainika kukiuka haki za watoto.

“Tutafanya msako mkali kwa kupita nyumba kwa nyumba kuwabaini wazazi wote waliowaficha ndani watoto wenye ulemavu na wale ambao umri wa kuanza shule umefika na hawajapelekwa shule, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao, kwani wanawanyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu.”

Amesema familia ambazo zimeshindwa kuwanunulia watoto wao sare za shule kutokana na ugumu wa maisha atashirikiana na uongozi wa kata hiyo, kuwanunulia ili wafanane na watoto wengine.

Diwani wa kata ya Rau, Manispaa ya Moshi, Stallone Malinda akizungumza na baadhi ya wazazi waliowapeleka watoto wao kujiandikisha shule ya msingi Rau, iliyopo Wilaya ya Moshi. Picha na Janeth Joseph

“Tumeweka utaratibu wa kushirikiana na uongozi wa serikali za mitaa na mabalozi kuhakikisha tunawafikia wale wazazi ambao wameshindwa kabisa kuwanunulia sare watoto wao ili tuone namna ya kuwasaidia,”amesema Diwani Malinda

Naye, Mwenyekiti wa mtaa wa Karikacha, Sweetfredy Maleo, amesema ataungana na diwani huyo kuhakikisha watoto wote wenye sifa ya kuandikishwa shule kwenye mtaa wake wanapata haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Rau, Prisca Mushi amesema mpaka kufikia jana wameandikisha wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza kwa zaidi ya asilimia 88.2.

“Shule hii ina jumla ya wanafunzi 643, jana wameripoti wanafunzi asilimia 88.2. Tulikuwa tunatarajia kuandikisha wanafunzi 68 darasa la awali, ambapo wavulana ni 32 na wasichana 36, lakini kufikia hiyo jana tumefanikiwa kufikia matarajio hayo,”amesema Mwalimu Mushi

Ofisa elimu wa kata hiyo, Mwalimu Vailet Msonde amesema wameendelea kushirikiana na wazazi kuhakikisha wanatoa michango ya chakula mashuleni ambapo hatua hiyo kwa kiasi kikubwa wanafunzi kufanya vizuri darasani.