Moshi. Wakati maswali mengi yakiibuka kuhusu utata wa kifo cha Michael Rambau (18) anayedaiwa kujinyonga kwa kutumia mkanda akiwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Moshi Kati, familia imekabidhiwa mwili kwa ajili ya taratibu za maziko.
Kijana huyo aliyekuwa fundi bomba na dereva bodaboda, mkazi wa Mtaa wa Karikacha, Kata ya Rau, mkoani Kilimanjaro anadaiwa kujinyonga kwa kutumia mkanda akiwa mahabusu alikokuwa akishikiliwa Januari 13, 2026 kwa tuhuma za kumjeruhi baba yake mdogo kwa kumpiga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 14, 2016 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, mtuhumiwa huyo alikuwa akituhumiwa kufanya tukio la mauaji ya baba yake mzazi Novemba 22, 2025 kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni kisha kutoroka hadi alipokamatwa Januari 13, kwa kosa la kumshambulia na kumdhuru baba yake mdogo, Brian Felix.
Akizungumza msemaji wa familia, ambaye ni baba mdogo wa kijana huyo, Today Rambau amesema tayari mwili wa kijana huyo umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi yatakayofanyika Jumamosi Januari 17.
“Mwili tayari umefanyiwa Postmortem (uchunguzi) na tunatarajia kuzika siku ya Jumamosi hapa nyumbani Rau, na taratibu zote zimekamilika,” amesema Rambau.
Alipoulizwa kuhusu majibu ya uchunguzi wa mwili wa marehemu alidai, polisi wanayo na wao ndio wanapaswa kujibu suala hilo.
“Majibu wanayo polisi,waulizeni wao watawapa,sisi tumewaachia kila kitu,”amesema Msemaji huyo
Pamoja na taarifa hiyo ya familia, utata uliojitokeza ni namna kijana huyo alivyoweza kuingia na mkanda mahabusu anaodaiwa kuutumia na kuukatisha uhai wake.
Mama wa merehemu, Ludovika Mushi, akilia kwa uchungu kufuatilia kifo cha mwanaye anayedaiwa kujiua kwa kujinyonga kituo cha polisi Moshi kati, Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Kiutaratibu mtuhumiwa anapokamatwa na Jeshi la Polisi kabla ya kuingizwa mahabusu hufanyiwa ukaguzi na kukabidhi vitu vyote ikiwamo mkanda, pesa, viatu, simu pamoja na vitu vingine, jambo ambalo limeibua maswali mengi kwa jamii.
Alipotafutwa kamanda wa polisi mkoani humo kujibu utata huo kuwa, ilikuwaje mtuhumiwa akaruhusiwa kuingia na mkanda mahabusu, simu yake iliita mara kadhaa bila kupokewa.
Akizungumza jana Jumatano na waandishi wa habari msemaji huyo wa familia alidai, taarifa walizopewa polisi ni kwamba kijana huyo anadaiwa kujiua kwa kutumia mkanda akiwa mahabusu.
“Nilipigiwa simu kwamba ndugu yetu amejiua kwa kujinyonga akiwa mahabusu na kwamba alitumia mkanda,” amesema baba mdogo huyo.
Akielezea sababu za kijana huyo kukamatwa, msemaji huyo wa familia amesema Januari 12 kijana huyo alitofautina na baba mdogo wake wakati alipochukua spana za gari la marehemu baba yake aliyefariki Novemba 22, mwaka jana.
“Michael (marehemu) alikamatwa Januari 13, kwa tukio la kumshambulia baba yake mdogo kwa kumpiga na bapa na kupelekwa kituo cha polisi,” amesema msemaji huyo wa familia
“Hili tukio ni tukio la mshtuko sana kwa sababu mtu amechukuliwa leo(Januari 13) halafu unapewa taarifa eti kajiua ndani ya mahabusu, hili sio jambo la kufurahisha hata kidogo,” amesema Rambau.
Awali, akizungumza mama wa marehemu, Ludovika Mushi alidai baada ya kijana huyo kutofautiana na baba yake mdogo, alienda Uru na wakati wakitafuta mwafaka wa tukio hilo, Jumatatu Januari 12, 2026, alipigiwa simu akitakiwa aende nyumbani Rau ili waweze kuzungumza na kuyamaliza.
“Alipoitwa aje nyumbani kwa mazungumzo ya suluhu, ndipo alikamatwa. Niliambiwa alikamatwa na polisi, aliachiliwa kwa dhamana, akarudi nyumbani, lakini baadaye akapigiwa simu akaambiwa arudi polisi. Jioni ndipo nikaambiwa mwanangu amefariki kwa kujinyonga,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu mwanaye kutoroka, amesema hakuwahi kuondoka nyumbani hapo tangu kifo cha baba yake na kwamba aliondoka nyumbani Alhamisi iliyopita baada ya kukorofishana na baba yake mdogo.
“Aliondoka nyumbani Alhamisi ya wiki iliyopita baada ya kutokea mvutano na baba yake mdogo, ndipo akaja Uru hadi aliporejeshwa nyumbani Rau kwa madai ya kwenda kusuluhisha mgogoro huo,” amesema mama huyo.