Mwanza. Kero ya utiririshaji wa maji taka na vinyesi kutoka katika maeneo ya milimani jijini Mwanza, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitishia afya na uchafuzi wa Ziwa Victoria inatarajiwa kuwa historia kufuatia kupanuliwa kwa Mradi wa Kipaumbele cha Juu cha Mwanza (Mwanza HPI).
Kupitia nyongeza ya makubaliano ya mradi na ufadhili uliosainiwa leo Alhamisi Januari 15, 2026, Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kwa kushirikiana na Serikali imeongeza wigo na fedha za mradi huo unaolenga kuboresha miunganisho ya mifumo ya majitaka hususan katika maeneo ya miinuko kama Igogo, Mabatini, Kirumba, Pasiansi na Nyamanoro.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire amesema baadhi ya wakazi wa jijini humo wanaoishi milimani, hawana mifumo salama ya majitaka hali inayosababisha maji machafu kutiririshwa ovyo kuelekea maeneo ya chini na hatimaye kuingia Ziwa Victoria.
“Jiji la Mwanza lina wakazi zaidi ya milioni 1.5, lakini sehemu kubwa hawana vyoo na mifumo salama ya majitaka. Zaidi ya asilimia 30 ya uchafu, ikiwemo vinyesi na maji taka ya majumbani na viwandani, huingia moja kwa moja ziwani,” amesema Dk Bwire.
Ameeleza kuwa hali hiyo siyo tu inaathiri afya za wananchi bali pia ni hatari kwa uhai wa Ziwa Victoria, akionya kuwa endapo uchafuzi utaendelea kwa kasi ya sasa, utafiti unaonesha ndani ya miaka 30 ijayo ziwa hilo linaweza kushindwa kuhimili viumbe hai wakiwemo samaki.
Amesema mradi uliopanuliwa unahusisha ujenzi wa kilomita 14.4 za mabomba ya ziada ya majitaka, ujenzi wa miunganisho mipya 1,600 kwa kaya na taasisi, pamoja na ukarabati wa vituo vya kusukuma majitaka na ununuzi wa magari ya kunyonya majitaka.
Mradi wa Mwanza HPI unatekelezwa chini ya Mpango wa Usimamizi Jumuishi wa Rasilimali za Maji wa Bonde la Ziwa Victoria (LVB-IWRMP) na unasimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Salama jiji la Mwanza (Mwauwasa), huku pia ukitarajiwa kutekelezwa katika miji mingine ya bonde hilo ikiwemo Kisumu (Kenya), Kampala (Uganda) na Kigali (Rwanda).
Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwauwasa, Neli Msuya (kulia) wakisaini nyongeza ya makubaliano ya mradi na ufadhili wa Mradi wa Kipaumbele cha Juu wa Mwanza (Mwanza HPI). Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amir Mkalipa akishuhudia tukio hilo.
“Desemba 2024, LVBC ilipokea misaada miwili ya ziada yenye jumla ya Euro milioni 30 kwa ajili ya kuunga mkono mpango huo. Baadaye, Machi 2025, makubaliano ya utekelezaji wa mpango huo yanayojulikana kama ‘Separate Agreements’ yalisainiwa kati ya Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) na LVBC, hivyo kuwezesha matumizi ya fedha za ziada,”amesema Dk Bwire.
Mkurugenzi wa Mwauwasa, Neli Msuya amesema katika awamu hii, mkazo mkubwa umewekwa katika ujenzi wa mifumo rahisi ya kukusanya majitaka kutoka makazi ya milima yanayozunguka jiji hilo.
“Jumla ya nyumba 1,800 zitaunganishwa zikiwemo taasisi na majengo ya biashara kama hoteli. Takribani kilomita 25 za mabomba zitalazwa, sambamba na ujenzi wa kituo kipya cha kusukuma majitaka,” amesema Msuya.
Ameongeza mradi huo pia utahusisha ununuzi wa magari mawili ya kunyonya majitaka, ujenzi wa maabara ya kufuatilia ubora wa majitaka, pamoja na ukarabati wa mabwawa ya kutibu majitaka, hatua zitakazosaidia kupunguza uchafu unaotiririka kuelekea mitaani na ziwani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa amesema mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza, kama siyo kuondoa kabisa, magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu yanayotokana na uchafu ukiwemo wa majitaka.
Amewataka wananchi waheshimu miundombinu akisisitiza mitaa itakayohujumu itachukuliwa hatua kali kwa kuwa itakuwa inarudisha nyuma jitihada za Serikali na wadau, huku akiitaka Mwauwasa kufanya manunuzi kwa kuzingatia sheria za nchi pamoja na ubora wa vifaa.
Mkazi wa Igogo, Anthony Gabriel amesema mradi huo utakapokamilika utaondoa kero kubwa ya maji machafu yanayotiririka kutoka milimani hasa wakati wa mvua.

