Kitendawili mauaji ya Happiness, Mwangobola aachiwa huru

Arusha. Ni nani aliyehusika na mauaji ya Happiness Fredrick, aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)? Swali hilo limeendelea kugubika jamii baada ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania kubatilisha hukumu ya kifo iliyokuwa imetolewa dhidi ya Idrisa Mwangobola, aliyekuwa mshtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji.

Happiness aliuawa Machi 18, 2019 katika eneo la Ungindoni Mjimwema, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, na mwili wake kuokotwa usiku huohuo katika eneo la Buza Sigara Relini. Tukio hilo lilisababisha mshtuko mkubwa kwa jamii, hususan kutokana na marehemu kuwa mwanafunzi mchanga wa chuo kikuu aliyekuwa na ndoto ya kuendelea na masomo yake Dodoma.

Baada ya uchunguzi, Mwangobola alifikishwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi ya jinai namba 75/2022. Mahakama hiyo ilimkuta na hatia ya mauaji na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa, ikiamini upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kosa hilo.

Hata hivyo, hukumu hiyo ilibatilishwa Desemba 17, 2025, na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walioketi Dar es Salaam ambao ni Mary Levira, Laila Mgonya na Gerson Mdemu. Mahakama hiyo iliruhusu rufaa ya mrufani na kuamuru aachiwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.

Katika uamuzi wao, majaji hao walikubaliana na hoja ya mrufani kwamba maelezo ya onyo yaliyotumiwa kama ushahidi muhimu yalirekodiwa kinyume cha sheria. Mahakama ilibaini mkanganyiko kuhusu ni nani aliyeyaandika maelezo hayo, iwapo yalielezwa ipasavyo kwa mrufani na kama yalisomwa kwake baada ya kuandikwa, jambo lililokiuka matakwa ya kisheria.

Jaji Gerson Mdemu alisema dosari hizo zilifanya maelezo ya onyo kuwa batili kisheria na hivyo kuondolewa kabisa katika kumbukumbu za rufaa. Kufuatia hatua hiyo, Mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi ya mrufani bila kuacha shaka yoyote.

Aidha, Mahakama ya Rufani ilifuta vielelezo vingine viwili vilivyodaiwa kuwa ni mali za marehemu vilivyokutwa katika chumba cha mrufani, ikibainisha kuwa vilipatikana kupitia upekuzi uliofanywa kinyume cha sheria. Baada ya kuondolewa kwa vielelezo hivyo, Mahakama ilibaini kuwa hakukuwa na ushahidi mwingine wa kimazingira au wa moja kwa moja ulioweza kumuunganisha mrufani na mauaji hayo.

Majaji hao pia walikosoa vikali upande wa mashtaka kwa kushindwa kumwita shahidi muhimu, Dorice, aliyedaiwa kuwa rafiki wa karibu wa marehemu na ndiye aliyetoa taarifa za awali zilizopelekea kukamatwa kwa mrufani. Mahakama ilieleza kuwa kushindwa kumwita shahidi huyo kuliacha pengo kubwa katika kesi upande wa mashtaka.

Katika kesi ya awali, upande wa mashtaka uliita jumla ya mashahidi tisa na kuwasilisha vielelezo vitano, huku mrufani akiwa shahidi pekee wa upande wa utetezi. Shahidi wa kwanza wa mashtaka alikuwa baba wa marehemu, Frederick Francis, aliyedai kuwa mawasiliano yake ya mwisho na binti yake yalikuwa Machi 18, 2019, baada ya marehemu kumweleza kuwa amekata tiketi ya basi la Kimbinyiko kwa ajili ya kurejea Dodoma siku iliyofuata.

Mashahidi wengine wa mashtaka walidai kuwa mrufani alikiri kumuua marehemu na kuutupa mwili wake, madai ambayo yalipingwa vikali na upande wa utetezi. Katika utetezi wake, mrufani alidai marehemu hakuwa mpenzi wake bali walikuwa mwanafunzi mwenzake wa zamani katika Shule ya Sekondari Jitegemee, na hakuwahi kukiri kumuua kama ilivyodaiwa.

Katika rufaa, mrufani aliwasilisha sababu sita ikiwemo upekuzi na ukamataji uliofanywa kinyume cha sheria, ushahidi dhaifu wa kimazingira na kushindwa kuthibitishwa kwa kesi bila kuacha shaka yoyote. Mahakama ya Rufani ilikubaliana na hoja hizo na kubatilisha hukumu ya Mahakama Kuu.

Uamuzi huo umeacha maswali mazito kwa jamii na familia ya marehemu kuhusu nani hasa alihusika na mauaji ya Happiness Fredrick, huku pia ukiibua mjadala mpana juu ya ubora wa uchunguzi wa kesi nzito za jinai nchini.