Malori ya Tanzania yadaiwa kutekwa Zambia, ofisi ya balozi yafafanua

Dar es Salaam.  Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo (Tamstoa) wamelalamikia kuongezeka kwa matukio ya kutekwa kwa malori yao na kuibiwa madini ya shaba na kopa nchini Zambia.

Balozi wa Tanzania nchini humo, Luteni Mathew Mkingule amesema ubalozi huo haujapokea taarifa rasmi kuhusu tukio lolote la aina hiyo.

Akizungumza kuhusu madai hayo, Balozi Mkingule amesema endapo matukio ya wizi au utekaji yametokea, wahusika wanapaswa kwanza kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama vya Zambia, hususan Jeshi la Polisi, ili uchunguzi uanze.

Amefafanua kuwa baada ya Polisi kupokea taarifa, ndipo wanapaswa kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania ili kutoa taarifa endapo kuna raia wa Tanzania aliyehusika au kuathiriwa.

“Wamiliki wa magari au wasafirishaji wanapaswa pia kuwasiliana na ubalozi ili kuanza mchakato wa ufuatiliaji. Hizi ndizo taratibu rasmi, sawa na ilivyo Tanzania ambapo tukio la wizi lazima liripotiwe Polisi kwanza,” amesema Mkingule.

Akieleza sababu za kuvunja ukimya wao, Dar es Salaam leo Januari 15, 2026 Mwenyekiti wa Tamstoa, Chuki Shabani, amedai vitendo vya kutekwa kwa malori yanayobeba shaba na kopa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenda Tanzania vimekithiri.

“Wanateka malori, wanaiba kopa na kuwapiga madereva. Ukijaribu kupinga unajeruhiwa. Shaba ikiibiwa, gharama za kulipa mzigo zinarudi kwa msafirishaji,” amesema Shabani.

Ameongeza kuwa katika baadhi ya matukio, madereva wamekuwa wakikamatwa na kuwekwa mahabusu wakishinikizwa kulipa thamani ya mizigo iliyoibiwa, huku akidai wamekuwa kimya kwa muda mrefu wakitarajia mamlaka husika kuchukua hatua bila mafanikio.

“Tatizo linaendelea kuota mizizi. Shaba na kopa vinaibiwa hata mchana kweupe. Kopa si ndogo, ni mapleti makubwa, lakini bado yanatekwa,” amesema.

Shabani amesema licha ya mizigo hiyo kuwa na walinzi wa wenye mizigo, lawama na gharama huangukia kwa dereva na mmiliki wa lori endapo wizi unatokea.

“Mmiliki anatakiwa kulipa mzigo wenye thamani hata ya zaidi ya Sh bilioni moja. Huu ni uonevu. Ndani ya mwezi huu pekee, malori mawili yamekamatwa na kuibiwa kopa,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Madereva Tanzania (TADWU), Ramadhani Selemani, amesema matukio hayo yamekuwa changamoto kubwa kwa madereva wanaosafirisha mizigo kupitia Zambia.

“Madereva wanavamia, wanapigwa, wanaumizwa na wengine wanafungwa. Hali hii husababisha migogoro kati ya dereva na mmiliki wa gari na kudhoofisha maisha na uchumi wa madereva,” amesema.

Ametoa wito kwa Serikali kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha usalama wa malori ya Kitanzania na kukomesha vitendo vya utekaji.

Katika hatua nyingine, Balozi Mkingule ameongeza kuwa katika baadhi ya matukio, madereva wamewahi kutuhumiwa kuwa chanzo cha matatizo kwa madai ya kuuza shaba wanaporejea.

ingawa amesisitiza kuwa yapo pia matukio halisi ya ujambazi na utekaji yanayohitaji uchunguzi wa kina kulingana na mazingira ya tukio.