Matokeo ya uchaguzi Uganda kujulikana ndani ya saa 72

Dar es Salaam. Zaidi ya wananchi milioni 21 nchini Uganda leo Alhamisi Januari 15, 2026 wanatarajiwa kupiga kura katika zaidi ya vituo 50,000 katika uchaguzi mkuu unaotajwa kuwa na mvutano mkali zaidi katika historia ya chaguzi za hivi karibuni nchini humo.

Mnyukano huo unatajwa kuwa umefanya uchaguzi kufanyika katika mazingira ya ulinzi mkali na tahadhari kubwa za kiusalama dhidi ya hofu ya migogoro ya kisiasa kutoka kwa wafuasi wa wagombea ambapo maofisa wa usalama wamesambazwa kwa wingi nchi nzima hasa jijini Kampala na maeneo mengine yenye ushindani mkubwa.

Asubuhi ya leo, wapigakura wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura huku ikielezwa kuwa mwamko ulikuwa mdogo katika baadhi ya maeneo, maofisa wa usalama wakitanda karibu kila eneo na magari ya doria kuzunguka mitaani.

Watu wanasubiri nyenzo za kupigia kura katika kituo cha kupigia kura mjini Kampala mnamo Januari 15, 2026. PICHA na ABUBAKER LUBOAA

Mbali na ulinzi huo, shughuli za kawaida zimeripotiwa kuendelea kila mahali hasa katika majiji makubwa huku idadi kubwa ya polisi ikielezwa kwa kiasi fulani kuwatia hofu wananchi.

Hali ya upigaji kura, mawakala

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema saa moja asubuhi, zoezi la kupiga kura lilipoanza rasmi na kuendelea hadi muda uliopangwa wa saa kumi jioni kwa saa za Uganda.

Tume ya Uchaguzi nchini humo imesisitiza kuwa wapiga kura wote watakaokuwa kwenye foleni ifikapo saa ya kufunga vituo wataruhusiwa kuendelea kupiga kura ili kutumkutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wa Taifa lao.

Aidha, kwa uapnde wa mawakala wa vyama mbalimbali nao wameripotiwa kuwasili vituoni kusimamia mchakato huo mapema na wameendelea kuwa vituoni kwa uda wote zoezi la upigaji kura likiendelea.

Maandalizi vifaa, kuzimwa intaneti

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, maandalizi ya upigaji kura yalikamilika tangu, jana, huku vifaa vya kupigia kura vikifikishwa katika vituo vyote kabla ya leo asubuhi.

Wakati wa maandalizi ya upigaji kura, Serikali ya Uganda imezima mtandao wa intaneti na kusitisha mawasiliano yote ya mitandaoni, hatua inayoelezwa kuwa imeibua malalamiko miongoni mwa wadau wa uchaguzi huo na jumuiya za kimataifa.

Afisa wa polisi na wanajeshi wanaonekana katika kituo cha kupigia kura mjini Kampala Januari 15, 2026, kabla ya uchaguzi wa kitaifa. PICHA/ABUBAKER LUBOWA

Wakosoaji wa hatua hiyo ya serikali kuzima mitandao tangu Jumanne Januari 13, 2025, kwa madai ya kudhibiti upotoshaji na uchochezi wa machafuko wakati na baadaya uchaguzi, wamesema hali hiyo inakwamisha mawasiliano na uratibu wa mawakala wa vyama pamoja na kuzuia ufuatiliaji huru wa umma katika mchakato wa uchaguzi.

Shirika la Amnesty International limetoa onyo kuhusu kuzimwa kwa mtandao likiitaka mamlaka nchini humo kurejesha huduma hiyo ya mawasiliano ili kuondoa usumbufu na haki ya wananchi kupata taarifa juu ya mwenendo wa uchaguzi wao.

Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Tigere Chagutah ameitaka Serikali kuachilia mtandao, akisema hatua hiyo ni ukandamizaji wa haki za binadamu na inakinzana na mikataba ya kimataifa.

Mapema asubuhi, Tume ya Uchaguzi nchini humo imetoa mwongozo mpya wa upigaji kura ikiwa ni tahadhari kuwa kama itatokea hitilafu ya vifaa vya kuthibitisha wapigakura kwa alama za vidole (BVVK), mchakato wa kupiga kura utaendelea kwa kutumia daftari la kitaifa la wapigakura.

Aidha, imewataka wananchi kujitokeza kutumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wao ikiwahakikishia kuwa haki yao italindwa na wote watakaokuwa kwenye foleni ya kupiga kura, hata ikifika muda wa kufungwa kwa vituo uliopangwa wa saa 10 jioni, wataendelea kukamilisha shughuli hiyo hiyo.

“Vituo vya kupigia kura vitaendelea kuwa wazi hadi wapigakura wote waliojiandikisha na waliopo kwenye foleni ifikapo saa 10 jioni wawe wamepiga kura zao,” ametangaza Mwenyekiti wa Tume hiyo, Simon Byabakama.

Afisa wa Tume ya Uchaguzi akitayarisha vifaa vya kupigia kura wakati upigaji kura ukiendelea Kampala, Uganda Januari 15, 2026. PICHA na ABUBAKER LUBOWA

Katika uchaguzi huo ambao Rais Yoweri Museveni (81) anatafuta muhula wa saba baada ya kutawala kwa zaidi ya miongo minne, akichuana na wagombea wengine saba, akiwemo mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, shughuli ya kuhesabu kura itaanza mara moja baada ya upigaji kura kukamilika.

Wakati macho na masikio ya ya Waganda na dunia yakigeukia sanduku la kura kujua hatima ya Museven, anayeungwa mkono na jamii za pembezoni na watu wa mlengo wa serikali akitetea kiti chake dhidi ya Bobi Wine, anayeungwa mkono na jamii za mijini na vijana, matokeo yanatarajiwa kutangazwa Jumamosi mchana.

Kiongozi wa Upinzani na mgombeaji urais wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP) Robert Kyagulanyi Ssentamu (Bobi Wine), anapiga kura mnamo Januari 15, 2026 katika Freedom Square huko Magere, Wilaya ya Wakiso. PICHA na ABUBAKER LUBOWA

Licha ya upigaji kura kufanyika kwa utulivu, wachambuzi wa siasa nchini Uganda wameendelea kuonyesha wasiwasi kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo wakionyesha mashaka kama haki itatendeka.

Maria Taremwa, mkazi wa Kampala, amesema uonevu na ukandamizaji ulioshuhudiwa wakati wa kampeni za uchaguzi huo dhidi ya wapinzani unatia mashaka kuhusu usimamizi wa haki katika uchaguzi huo.

“Watu wanapigwa mitaani hasa wapinzani na limetolewa agizo la kuwataka wapigakura kuondoka kwenye vituo mara baada ya kupiga kura, hii inaweza kuongeza mvutano kwani wengi wanataka kulinda kura zao,” amesema.

Pia, amesema kuzimwa kwa mtandao hasa Facebook, ni vikwazo vinavyozuia uhuru wa maoni.

Kwa upande wake, Jacob Nuwashumbusha, mkazi wa Kampala, ameonya kuhusu hatari ya kutokea vurugu ikiwa haki haitatendeka katika uchaguzi huo, akiwataka wanasiasa hasa wagombea kuwahimiza wafuasi wao kuwa watulivu.

Rais Museveni akipiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Upili ya Karo huko Rwakitura Januari 15, 2026. PICHA/SCREEN-GRAB/UBC

“Kwa kawaida nisingetarajia mlipuko wa vurugu, lakini tumekaa juu ya pipa la baruti ili kuepuka mlipuko huo, viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwahimiza wafuasi wao kuwa watulivu,” amesema.