Mbarawa: Jengo la watu mashuhuri JNIA limechochea biashara Dar

Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema jengo la watu mashuhuri katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal One) limechochea kasi ya shughuli za kibiashara jijini Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Januari 15, 2026, wakati wa maandalizi ya uzinduzi unaotarajiwa kufanyika kesho, Mbarawa amesema ujenzi wa jingo hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuboresha huduma na miundombinu ya usafiri wa anga nchini.

“Ujenzi wa jengo hili kwa kiwango kikubwa umechangia kuongeza mzunguko wa biashara katika Mkoa wa Dar es Salaam,” amesema Profesa Mbarawa.

“Jengo hili jipya na la kisasa linatarajiwa kuzinduliwa kesho na mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi. Linajumuisha kumbi tano za viongozi wa kimataifa, zikiwemo kumbi mbili za mikutano na ukumbi mmoja wa kusubiri,” ameongeza Profesa Mbarawa.

Ameeleza kuwa jengo hilo limefungwa vifaa vya kisasa vya umeme, maji, Tehama, mifumo ya zimamoto pamoja na viyoyozi, huku akibainisha kuwa ujenzi wa mradi huo ulikamilika rasmi Oktoba 31, 2025.

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, utekelezaji wa mradi huo ulizalisha ajira rasmi na zisizo rasmi kwa Watanzania takribani 1,010, sambamba na kutoa fursa kwa wakandarasi wa ndani kutumia vifaa vinavyopatikana nchini, ikiwemo nondo na kokoto.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa jengo jipya na la kisasa la watu mashuhuri lenye hadhi ya kutoa huduma kwa viongozi wa ngazi ya Urais, lililojengwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal One).

Jengo hilo lenye ghorofa moja linajumuisha kumbi tano kwa ajili ya viongozi wa kimataifa, zikiwemo kumbi mbili za mikutano na ukumbi mmoja wa kusubiri, likiwa na miundombinu ya kisasa inayokidhi viwango vya kimataifa.

Akitaja manufaa ya jengo hilo, Profesa Mbarawa amesema litasaidia kuwezesha mapokezi ya heshima kwa wageni wenye hadhi ya Urais, kutoa faragha kwa viongozi hao mashuhuri, pamoja na kuwa na eneo la kusubiri lenye miundombinu ya kisasa.

Pia, amesema jengo hilo linatarajiwa kuongeza mapato ya nchi, kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na kuongeza idadi ya miruko ya ndege nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uhandisi na Matengenezo, Focus Kadeghe amesema huo ni muendelezo wa Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga katika viwanja vyote nchini mathalani kwa viwanja viwili vya kimataifa.

“Shughuli ya uzinduzi itafanyika kesho kuanzia saa 2 Asubuhi. Mradi huu ulijengwa kwa siku 77 kwakuwa kila kitu kilikwepo ikiwemo vifaa na uharaka huo ulitokana na mpango huo ulikwepo kwa muda mrefu,” amesema.