Dodoma. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ametoa maagizo 17 kwa watendaji wa wizara na taasisi zilizo chini yake, huku akisisitiza hatamvumilia mzembe badala yake atamlinda atakayetoa maamuzi ya haki.
Miongoni mwa maagizo hayo ni kuwepo kwa matumizi ya mifumo inayosomana katika taasisi zote, ubora wa huduma za matibabu, kuwa na malengo ya lazima ili mpango wa bima ya afya kwa wote usiwe zimamoto bali endelevu. Pia alipiga marufuku matumizi makubwa ya Sh20 bilioni kwa ajili ya mitihani akitaka yakomeshwe mara moja.
Waziri Mchengerwa alitoa maagizo hayo jana Januari 14, 2026 wakati akihutubia kwenye kikao kazi baina yake na watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya na watumishi wa afya wa Mkoa wa Dodoma ambacho kilifanyika jioni katika viwanja vya Hospitali ya Benjamini Mkapa.
Washiriki kwenye mkutano huo walikuwa ni Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bohari ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wakurugenzi wa hospitali za kanda na hospitali ya Taifa, waganga wakuu wa mikoa na watumishi kutoka Wizara ya Afya.
Katika hotuba yake alisema kila kiongozi kwenye taasisi yake lazima awe na uthubutu.
“Naagiza hayo, lakini lazima tuangalie wakati wa kuanzisha bima ya afya kutakuwa na hatari ya kuwa na bidhaa bandia je, hilo tunaliona na kama ndiyo tumejipangaje, lazima tusimame juu ya msingi imara ili jambo hili lisiwe la zimamoto kama nchi nyingine zilizoanzisha kwa haraka lakini hawakudumu, huu siyo mradi wa muda mfupi,” amesema Mchengerwa.
Amesema suala la bima ya afya kwa wote halipaswi kupimwa kwa muhula mmoja wa uongozi badala yake tathimini iwe ya muda mrefu kidogo na kutaka mwanzo wa yote uwe ni kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, na uwezo wa kuhudumia wagonjwa ili kuondoa manung’uniko.
“Nataka sekta ya afya itambulike kwa vitendo siyo mawasilisho ya maandishi, hospitali zisitegemee mtu mmoja ila kuwe na mfumo madhubuti kwani maeneo mengi naona matatizo yanakuwa maarufu wakati mwingine hata kuzidi masuluhisho, sitarajii kuona hilo,” amesema na kuongeza.
“..sitavumilia uzembe, wala uzembe hautakuwa ajali ya bahati mbaya, hapa wengi mtasema ni maneno tu, nataka kuwaambia katika hili hakutakuwa na mashinikizo ya kisiasa bali vitendo vitasimama hivyo msiongoze wenzenu kwa woga na hofu ya kulaumiwa, penye ukweli nitawalinda.”
Alisema uzinduzi wa bima ya afya kwa wote utafanyika ndani ya kipindi cha siku 100 za Rais Samia hapo huduma itaanza kutolewa.
Katika hatua nyingine alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe kufanya mapitio ya mabaraza ya nidhamu ili waanze kuwawajibisha wazembe, kikiwamo kitengo cha majengo alichosema hakiwajibiki, kwani wameacha majengo yaliyopo jirani na Hospitali ya Mloganzila hadi yamekuwa magofu.
Maagizo mengine kwa katibu ni muundo na mfumo wa vyuo vya afya vya Serikali kwani havizalishi wataalamu wazuri kama ilivyo kwa vyuo binafsi…“Nataka kujua tatizo nini, watumishi wondokaneni na kauli ya tumefanya kwa kadri ya uwezo wetu, kumbukeni kinachoangaliwa ni ubora wa huduma ambao umetolewa kwa wakati.”
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Edward Hosea alimwambia waziri kuna kilio cha nyumba za watumishi ambacho kinasababisha wengi kuishi mbali jambo linalopelekea kuwa na shida hasa inapotokea dharura hospitalini.
Profesa Hosea alimwomba Mchengerwa kuzitazama hospitali za kanda kwa kuzitengea bajeti toshelevu ikiwemo ya Benjamin Mkapa. “Kumekuwa na kilio cha mfumo wa maji kwa muda mrefu hivyo kuwa na hitaji la Sh3.5 bilioni kwa ajili ya kufunga mifumo ya kuchuja maji lakini hospitali imekusanya mapato ya ndani Sh600 milioni ambazo hazitoshi.”
Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi alimwambia Waziri kuwa wanakabiliwa na changamoto ya kifedha kwa ajili ya kuanzisha huduma za magonjwa ya saratani ambapo zinatakiwa jumla ya Sh30.1 bilioni, na upanuzi wa majengo ya kutoa huduma za magonjwa ya figo na upandikizaji uroto.
Profesa Makubi aliyataja mafanikio waliyofikia ni upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 54, upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 50 na idadi kubwa ya watoto waliopatiwa matibabu ya upandikizaji uroto, jambo lililofanya waokoe fedha nyingi ambazo zingetumika kwenda kupata matibabu nje ya nchi.
