Tanga. Utafiti umebaini kuwa mikataba mibovu ya mauzo ya mazao ndiyo chanzo kikubwa cha wakulima wa machungwa kuuza mazao yao kabla hayajakomaa, hali inayowanyima faida halisi na kuwaacha katika mzunguko wa umaskini wa kudumu.
Utafiti huo uliofanyika mwaka 2025, ukihusisha wadau wa ndani na nje ya nchi, umeonesha kuwa wakulima wengi huuza machungwa yakiwa bado kwenye hatua ya kutoa maua kutokana na uhitaji wa fedha za haraka, hali inayowalazimu kukubali bei ndogo zisizoendana na gharama za uzalishaji.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo katika kikao cha majadiliano kilichowakutanisha wadau kutoka Tanzania, Afrika Kusini, Kenya, Zambia, Malawi, Uingereza na Jamhuri ya Czech, Profesa Stephen Whitfield wa Health Research Project amesema mikataba hiyo inawanufaisha zaidi wanunuzi na kuwaweka wakulima kwenye mtego wa kifedha unaowazuia kunufaika na kazi zao.
Amesema kuuza machungwa kabla hayajakomaa ni hatari kubwa kwa mkulima, kwani endapo mnunuzi atachelewa kuvuna, mazao huweza kuharibika bila mkulima kuwa na haki ya kuyauza kwa mnunuzi mwingine kutokana na masharti ya mkataba wa awali.
Utafiti huo pia umebaini kuwa sehemu kubwa ya machungwa yanauzwa kwenye masoko ya nje ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Congo na Burundi, huku wakulima wengi wakiwa hawana taarifa kuwa mazao yao yanafika kwenye masoko ya kimataifa, jambo linalowanyima fursa ya kunufaika na bei ya ushindani.
Akichangia mjadala huo, Profesa Fortunata Makene wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii Tanzania (ESRF) amesema mfumo wa sasa wa masoko unawanufaisha zaidi madalali, huku mkulima mdogo akibeba mzigo mkubwa katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya machungwa.
Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Muheza, Silivesta Mzirai, amesema Serikali imeanza kuhimiza uundwaji wa vyama vya ushirika na umoja wa wakulima wa machungwa ili kuwawezesha kupata masoko ya pamoja, mikopo na kupunguza utegemezi kwa madalali.
Naye mkulima wa machungwa kutoka Mashewa, wilayani Korogwe, Aisha Waziri, amesema wakulima wengi huingia kwenye mikataba hiyo mibovu kwa kulazimika kutokana na hali ngumu ya maisha, akiiomba Serikali kuweka mifumo itakayowalinda wakulima wadogo dhidi ya unyonyaji.
