Serikali imejipanga kuwezesha upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika zao la kahawa, kwa lengo la kuchimba visima katika maeneo yenye changamoto ya uhaba wa maji. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha zao la kahawa linaendelea kuwa na tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa katika majadiliano na hafla ya kuhitimisha Mradi wa Utafiti wa PACSMAC, unaolenga kuelewa kwa undani changamoto na fursa katika sekta ya kahawa inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huo unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Idara ya Jiografia kwa kushirikiana na watafiti kutoka Ethiopia, Marekani, Uswisi pamoja na Shule ya Biashara ya Copenhagen (CBS) ya Denmark.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 15, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera, Utafiti na Ubunifu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Adella Ng’atigwa, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo, amesema ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo, watunga sera na wakulima utasaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika uzalishaji wa kahawa.
Ameongeza kuwa tafiti mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kupata mbegu bora za kahawa zinazostahimili magonjwa na ukame, hatua itakayoongeza tija na uzalishaji wa zao hilo.
Dkt. Ng’atigwa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi nne bora barani Afrika kwa uzalishaji wa kahawa, huku zaidi ya asilimia 90 ya wazalishaji wakiwa ni wakulima wadogo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Ruzuku za Miradi UDSM, Dkt. Leonard Binamungu, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Utafiti na Machapisho wa chuo hicho, amesema ushirikiano wa kimataifa unaongeza ubora wa tafiti na kutoa mitazamo mbalimbali inayosaidia kufanya matokeo ya utafiti kuwa ya kuaminika zaidi.
Ameeleza kuwa Tanzania na Ethiopia zimechaguliwa katika utafiti huo kutokana na umuhimu wa zao la kahawa katika nchi hizo mbili.
Lengo ni kubaini changamoto katika mnyororo wa thamani wa zao hilo na kuona kama ushahidi wa utafiti kutoka nchi hizo unaweza kusaidia kuboresha sekta ya kahawa barani Afrika kwa ujumla.
Aidha, wakulima wa kahawa nchini wameanza kunufaika na mpango wa Serikali wa ugawaji wa miche bora bure, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa kahawa na kuinua kipato cha wakulima.