Na Mwandishi wa OMH
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH)
leo, Januari 15, 2026 imeendesha semina maalumu kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) katika Ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma.
Semina hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa
utaratibu wa Bunge wa kuzijengea uelewa mpana kamati zake, ili kuziwezesha
kutekeleza majukumu ya kibunge kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia maslahi
mapana ya Taifa.
Semina hiyo imelenga kuijengea Kamati ya
PIC uelewa wa kina kuhusu muundo, majukumu na mwelekeo wa kimkakati wa Ofisi ya
Msajili wa Hazina katika usimamizi wa uwekezaji wa Serikali, sambamba na
uwasilishaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa miaka 25 (2026–2050).
Kupitia utaratibu huu wa Bunge, Kamati
hupata fursa ya kuelewa kwa undani majukumu, changamoto na mipango ya taasisi
wanazosimamia, jambo linalosaidia kuimarisha ubora wa maamuzi, usimamizi na
ushauri wa kibunge.
Katika mawasilisho yake, OMH imeeleza
historia ya kuanzishwa kwake tangu mwaka 1959, msingi wake wa kisheria chini ya
Sheria ya Msajili wa Hazina Sura ya 370, pamoja na mageuzi ya kimuundo na
kisheria yaliyofanyika ili kuiwezesha Ofisi kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi katika mazingira ya sasa ya kiuchumi, kibiashara na kiutawala.
Kamati imeelezwa kuwa OMH inatekeleza majukumu
yake makuu katika maeneo manne ya msingi ambayo ni kumiliki na kuhifadhi mali
za Serikali kwa niaba ya umma, kuishauri Serikali kuhusu uwekezaji na usimamizi
wa mashirika ya umma, kusimamia utendaji kazi wa taasisi na mashirika hayo,
pamoja na kusimamia urekebishaji na ubinafsishaji pale inapohitajika.
Aidha, ilisisitizwa kuwa jukumu la msingi
la Ofisi ni kuhakikisha mashirika ya umma yanachangia kikamilifu katika Mfuko
Mkuu wa Serikali kupitia mapato yasiyo ya kodi, sambamba na kupunguza utegemezi
wa ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Katika muktadha huo, Kamati ya PIC
imeelezwa kuhusu muundo mpya wa OMH ulioboreshwa mwaka 2023 unaojumuisha
Kurugenzi tisa na Vitengo vitano, muundo unaolenga kuimarisha uwajibikaji,
kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuendana na ongezeko la idadi ya mashirika ya
umma pamoja na mabadiliko ya kiteknolojia na kiuchumi.
Sehemu muhimu ya semina hiyo ilikuwa ni
uwasilishaji wa Mpango Elekezi wa Muda Mrefu wa OMH kwa kipindi cha 2026 hadi
2050. Kupitia mpango huo, OMH imebainisha dhamira ya kuongoza mageuzi ya
kiuchumi kwa kusimamia uwekezaji wa Serikali kwa mtazamo wa muda mrefu,
unaozingatia tija, uwajibikaji na uendelevu, sambamba na utekelezaji wa Dira ya
Maendeleo ya Taifa 2050.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Msajili
wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, ametoa wito kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu na wa dhati
kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina katika kusimamia na kuongoza mageuzi ya muda
mrefu ya uwekezaji wa umma.
Ameeleza kuwa mafanikio ya Mpango Elekezi
wa Muda Mrefu na mageuzi yanayolengwa hayawezi kupatikana bila usimamizi
madhubuti, mwongozo wa kisera na uungwaji mkono wa Bunge kupitia Kamati husika.
Bw. Mchechu amesisitiza umuhimu wa
ushirikiano huo katika kuoanisha mifumo ya kisheria na kitaasisi, kuimarisha
utawala bora katika bodi na menejimenti za mashirika ya umma, pamoja na kuweka
mazingira wezeshi yatakayoiwezesha OMH kusimamia uwekezaji wa Serikali kwa
misingi ya kibiashara, uwajibikaji na ushindani.
Aidha, amebainisha kuwa Kamati ya PIC ina
nafasi ya kipekee ya kuhakikisha mageuzi haya yanapata mwendelezo na uthabiti
kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina ametoa
ahadi kwa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuwa ofisi yake
itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu, taarifa kwa wakati na ushauri wa
kitaalamu ili kuiwezesha Kamati kutekeleza majukumu yake ya kibunge kwa
ufanisi.
Ameahidi kuwa OMH itaendelea kuwa wazi, tayari
kushirikiana na Kamati katika masuala ya ufuatiliaji, tathmini na usimamizi wa
uwekezaji wa umma, pamoja na kutoa ufafanuzi na taarifa zote muhimu
zitakazohitajika katika utekelezaji wa majukumu ya kibunge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PIC, Mhe.
Masanja Kadogosa, alieleza matarajio yake ya kuona utekelezaji thabiti wa
majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) unaoleta matokeo yanayopimika,
hususan katika kuimarisha utendaji wa mashirika ya umma, kuongeza mapato yasiyo
ya kodi, na kupunguza utegemezi wa mashirika hayo kwenye ruzuku ya Serikali.
Ujumbe mkuu kutoka kwa Bw. Kadogosa, pamoja
na wajumbe wengine wa kamati, ni wito kwa mashirika ya umma kuzalisha kwa tija
ili kuchangia katika pato la taifa na kuboresha maisha ya wananchi
“Tunatarajia kuona uwazi, utawala bora na
uwajibikaji katika usimamizi wa uwekezaji wa umma,” alisisitiza, huku akisema,
“sisi kama kamati, tupo tayari kuisaidia Ofisi ya Msajili wa Hazina kutekeleza
mageuzi katika mashirika ya umma.”