NAOT yatangaza ajira 142, wahitimu kada mbalimbali waitwa kuomba

Dar es Salaam. Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imetangaza nafasi 142 za ajira kwa Watanzania wenye sifa, hatua inayolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa ofisi hiyo katika kusimamia uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

Tangazo hilo limetolewa mwanzoni mwa wiki hii, kupitia Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa niaba ya NAOT, likiwaalika wahitimu wa kada mbalimbali kuwasilisha maombi yao kabla ya Januari 24, 2026.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, nafasi nyingi zaidi ni za Mkaguzi Daraja la II, ambapo nafasi 121 zimetengwa kwa wahitimu wa fani za uhasibu na fedha, ikiwemo shahada ya uhasibu, uhasibu na fedha, uhasibu na teknolojia ya habari na uhasibu wa sekta ya umma.

Majukumu ya wakaguzi hao ni pamoja na kushiriki kuandaa na kutekeleza mipango ya ukaguzi, kukagua hati za malipo na akaunti za benki, kufanya uchunguzi wa mifumo ya udhibiti wa ndani, kuandaa hoja na taarifa za ukaguzi, pamoja na kushirikiana na taasisi zinazokaguliwa ili kuhakikisha ukaguzi unatekelezwa kwa ufanisi.

Mbali na kada ya uhasibu, NAOT pia imetangaza nafasi katika fani maalumu zinazohusiana na ukaguzi wa sekta mbalimbali. Fani hizo ni udaktari wa mifugo, famasia, afya ya jamii, uhandisi wa maji na umwagiliaji na uhandisi wa mazingira.

Nyingine kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni uhandisi wa umeme, uhandisi wa ujenzi, usanifu wa majengo, ukadiriaji wa ujenzi, usanifu na matumizi ya ardhi, sayansi ya taarifa za kijiografia (Geoinformatics), sayansi ya takwimu za bima na menejimenti ya kodi.

Katika eneo la mawasiliano, NAOT pia imetangaza nafasi mbili za ofisa habari daraja la II, moja katika fani ya uandishi wa habari na nyingine katika ubunifu wa michoro.

Aidha, imesema waombaji wa nafasi hizo wanatakiwa kuwa na shahada husika katika uandishi wa habari, mawasiliano ya umma au teknolojia ya multimedia na ubunifu wa michoro.

Kwa fani za uhandisi na taaluma za kitaaluma zinazodhibitiwa na mabaraza ya kitaaluma, waombaji wanatakiwa wawe wamesajiliwa na bodi husika ikiwemo Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Wafamasia Tanzania (PC), Baraza la Veterinari Tanzania (VCT) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

Tangazo hilo, linasisitiza kuwa utoaji wa taarifa au sifa za kughushi utachukuliwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika. Waombaji wote wanatakiwa kuwasilisha maombi yao kupitia mfumo wa kielektroniki wa ajira.

Aidha, waombaji wanakumbushwa kuambatisha barua ya maombi iliyosainiwa pamoja na vyeti vya elimu, huku barua hizo zikielekezwa kwa Katibu, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.