Serikali kumchukulia hatua mkandarasi barabara Kahama

Kahama. Serikali imesema itachukua hatua za kisheria dhidi ya mkandarasi Sichuan Road and Bridge Group (SRBG) anayetekeleza ujenzi wa barabara na mifereji ya maji katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, kutokana na kuchelewesha utekelezaji wa kazi kinyume na makubaliano ya mkataba.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi, Rogatus Mativila, Januari 15, 2026, wakati timu ya wataalamu wa Tamisemi ilipotembelea mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mpango wa Uboreshaji Miji Tanzania (Tactic) ili kuufanya tathmini.

Mhandisi msimamizi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Samuel Mtuwa (kulia), akitoa maelezo ya mradi kwa Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia miundombinu ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi Rogatus Matilila (kushoto), leo Januari 14, 2026. Picha na Amina Mbwambo

Mativila amesema maendeleo ya mradi hayaridhishi, huku mkandarasi akiomba muda wa nyongeza mara kwa mara, ingawa tayari ameshalipwa zaidi ya asilimia 20 ya thamani ya mkataba. “Leo Januari 15 ndio mwisho wa muda ulioongezwa wa siku 230. Sasa tutaketi kupitia ripoti na mkataba wake kuona kama tunaweza kuendelea naye au kumvua kazi na kumpatia mkandarasi mwingine,” amesema.

Amesema sababu zilizotolewa na mkandarasi ikiwemo mvua, maji karibu na changamoto za kupata lami hazitoshi kama msingi wa kuchelewesha kazi. Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amekiri mradi kucheleweshwa huku wananchi wakipata adha, hasa kipindi cha mvua. “Hadi sasa, mkandarasi ameweka lami kilomita moja kati ya kilomita 12 zinazohitajika,” amesema.

Sehemu ya mfereji wa maji unaotarajiwa kukusanya maji ya mvua ya ukanda wa juu Malunga na Busoka, kuondoa adha ya maji kwenye makazi ya watu yaliyopo ukanda wa chini ikiwemo kata ya Majengo na Mhongolo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga. Picha na Amina Mbwambo

Wakazi wa Kahama, wakiwemo Sofia Mbacha na Simon Mabumba, wamesema barabara na mitaro iliyopo ni hatari. Mbacha amesema, “Mvua inanyesha, nyumba zinaweka ufa, na kama mtu hana moramu au mifuko ya kulinda maji nyumba inaweza kuanguka. Wanaenda polepole mno.” Mabumba ameongeza kuwa watoto wanapopita barabara hiyo kwenda shule wapo hatarini kutokana na kuwapo kwa korongo kubwa bila daraja.