Serikali yatangaza ajira 1,200 kada mbalimbali

Dar es Salaam. Serikali imetangaza ajira 1,283 zinazohitajika kujazwa katika taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali pamoja na mamlaka za serikali za mitaa.

Kulingana na tangazo la ajira lililotolewa na Sekretarieti ya Ajira, nafasi nyingi zaidi ni za walimu wa Daraja la III C.
Takribani nafasi 709 zimetengwa kwa walimu wa hisabati, huku nafasi 201 zikiwa za walimu wa fizikia. Hatua hii inalenga kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi nchini.
Walimu hao watapangiwa ngazi ya mshahara ya TGTS-D kulingana na miongozo ya utumishi wa umma.

Aidha, Serikali imetangaza pia nafasi mbili za mlezi wa watoto msaidizi kwa ajili ya kuimarisha huduma za malezi, makuzi, na maendeleo ya awali ya mtoto.

Nafasi hizo ziko kwenye ngazi ya mshahara TGS-B na zinawalenga wahitimu wa mafunzo ya elimu ya awali, ustawi wa jamii, au saikolojia kutoka vyuo vinavyotambulika na Serikali.

Kwa upande wa taasisi za umma, kama Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira).

Nyingine ni Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (Tafori), Kituo cha Teknolojia ya Mitambo ya Kilimo na Maendeleo ya Vijijini (Camartec), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Nafasi nyingine zimetangazwa kwa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika (CAWM), na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma (PSRS), zimetangaza ajira 208 kwa kada mbalimbali.

Kwa taasisi ya Tawa, nafasi zilizotangazwa ni Askari Uhifadhi Daraja la III – Usimamizi wa Wanyamapori (nafasi 24), Askari Uhifadhi Daraja la III – Fundi Mitambo (nafasi 2),

Askari Uhifadhi Daraja la III – Fundi Famasi (nafasi 2), Askari Uhifadhi Daraja la III – Dereva (nafasi 6), Askari Uhifadhi Daraja la III – Katibu wa Ofisi (nafasi 3), na Askari Uhifadhi Daraja la III – Mwendesha Mitambo (nafasi 1).

Tasac  imeweka nafasi za Ofisa Usanifu wa Meli Daraja la II (nafasi 6), Ofisa Udhibiti wa Bendera na Bandari Daraja la II (nafasi 13), na Mwongozaji wa Boti Daraja la II (nafasi 9).

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetangaza nafasi za Ofisa Tehama Daraja la II (Programu) (nafasi 1), Mtakwimu Daraja la II (nafasi 20), na Ofisa Tehama Daraja la II (Programu) (nafasi 2).

TIRA imetangaza nafasi za Ofisa Bima Daraja la II (Bima ya Afya) (nafasi 2), TCAA nafasi za Ofisa Usimamizi wa Usafiri wa Anga Daraja la II (nafasi 17), na NIC nafasi za Ofisa Aktuari Daraja la II (nafasi 2) pamoja na Ofisa Bima Daraja la II – Madai (nafasi 2).

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimeweka nafasi za Mhadhiri Msaidizi – Uchakataji wa Mawimbi ya Kidijitali (nafasi 1), Mhadhiri Msaidizi – Utawala wa Biashara (nafasi 1), Mhadhiri Msaidizi – Usafirishaji na Usimamizi wa Ugavi (nafasi 1), na Mhadhiri Msaidizi – Elimu ya Biashara (nafasi 2).

Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika kimeweka Mhadhiri Msaidizi – Uhasibu/Fedha (nafasi 1), Mhadhiri Msaidizi – Utalii (nafasi 2), Msaidizi wa Mafunzo – Usimamizi wa Mazingira na Taka (nafasi 1), na Msaidizi wa Mafunzo – Usimamizi wa Wanyamapori (nafasi 1).

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeweka nafasi mbalimbali 20 za wahadhiri wasaidizi ikiwemo msaidizi wa mafunzo, Mhadhiri Msaidizi,, Ofisa Utawala, Ofisa Rasilimali Watu, Ofisa Mipango, Ofisa Manunuzi na Ugavi,ofisa Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) Mhasibu,Mkaguzi wa Ndani (Internal Auditor),Msaidizi wa Ofisi.

Nayo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) imetangaza nafasi 142, nyingi zaidi ni za Mkaguzi Daraja la II, ambapo nafasi 121 zimetengwa kwa wahitimu wa fani za uhasibu na fedha, ikiwemo shahada ya uhasibu, uhasibu na fedha, uhasibu na teknolojia ya habari, na uhasibu wa sekta ya umma.

Kulingana na tangazo la Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, kwa niaba ya taasisi zote zilizotangaza nafasi, ajira hizo zinapaswa kuombwa kabla ya mwisho wa Januari mwaka huu.