Tanroad watumia Sh9.9 bilioni ujenzi madaraja Lupa-Bitimanyanga, DC Chunya aonya wananchi

Mbeya. Zaidi ya Sh9.9 bilioni zimetumika kutekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa madaraja mawili ya Lupa na Bitimanyanga Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya.

Mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Barabara (Tanroad), Mkoa wa Mbeya kwa ufadhili wa Benki ya Dunia unatajwa kuleta chachu ya kiuchumi kwa wananchi na kuchangia mapato ya Serikali.

Meneja wa Tanroad Mkoa wa Mbeya, Suleiman Bishanga amesema utekelezaji wa miradi hiyo inakwenda kuchochea fursa za kiuchumi kwa wananchi hususani kusafirisha mazao kutoka Mbeya, Songwe na Rukwa kupelekea Tabora na Singida kupitia barabara ya Makongoro Wilaya ya Chunya.

Bishanga ameyasema hayo Jumatano Januari 14,2026,wakati wa ziara ya kukagua miradi hiyo ikihusisha wataalamu kutoka makao makuu ya   iliyoongozwa na Mtaalamu wa kitengo cha ushauri wa miradi Tanroad makao makuu,  Emmanuel Tang’ale ambaye alimwakilisha Meneja wa kitengo hicho kwa niaba ya Mtendaji Mkuu, Mohamed Besta.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo Bishanga amesema, miradi hiyo imetekelezwa kupitia mkandarasi Mzawa wa Kampuni ya Sama Contract ambayo imekidhi ubora wa viwango na kulingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali huku zaidi ya vijana 1,000 wamenufaika na ajira.

” Gharama za mradi wa daraja la Lupa Sh5.6 bilioni, sambamba na ujenzi wa matoleo yenye urefu wa kilomita sita na ufungaji wa taa 30, huku la Bitimanyanga limegharimu Sh4.3 bilioni na matoleo yenye urefu wa kilomita 25,na kufunga taa 42,”amesema.

“Barabara ya Makongoro kwenda Rungwa ina urefu wa kilomita 182, ambayo iko kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami itaunganisha mikoa ya Singida na Tabora na kuwa lango la fursa za kiuchumi kwa usarishaji wa bidhaa, “amesema.

Mwonekano daraja la awali ya Lupa Wilaya ya Chunya ambalo lilikuwa kikwazo kwa wananchi kukwamisha shughuli za kiuchumi kipindi cha mvua. Picha na Hawa Mathias

Bishanga amesema mikakati ya Serikali ni kuhakikisha inaboresha mawasiliano kwa kujenga miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami katika kutelekeza Ilani ya uchaguzi 2025/30.

“Kwa juhudi za makusudi za Rais Samia Suluhu Hassan tayari ametoa maelekezo ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami hususani ukamilishaji wa madaraja makubwa ya Lupa na Bintimanyanga ,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali itaendelea kuboresha miradi ya kimkakati ukiwemo wa barabara kuu ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia (Tanzam).

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga amesema miradi hiyo ya madaraja ya kimkakati ambayo italeta chachu kwa kufanya Wilaya hiyo kuwa lango la ukuaji wa uchumi na mapato ya Serikali.

Wakati huohuo, Batenga ameonya wananchi kuachana na tabia ya uharibifu  wa miundombinu ya madaraja na taa za barabarani ambayo Serikali inatumia gharama kubwa jambo ambalo halitavumilika.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Tanroad Makao Makuu,   Emmanuel Tang’ale amesema wameridhishwa na utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa madaraja ya Lupa na Bintimanyanga Wilaya ya Chunya.

Mwonekano wa daraja jipya la Lupa Wilaya ya Chunya lililoanza kutumika kwa wananchi wa Mikoa ya Mbeya, Singida na Tabora. Picha na Hawa Mathias.

Mkazi wa Lupa, Zaitun Hassan amesema maboresho ya miundombinu hiyo yataleta chachu katika shughuli za kiuchumi tofauti na awali.

“Awali tulikuwa tunapata changamoto hususani kwa wajawazito wakati wa kwenye kliniki katika msimu wa mvua ,kimsingi tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita,” amesema.

Naye Dereva bodaboda, Sham Joseph amesema licha ya ujenzi wa madaraja wanaomba Serikali kuharakisha kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuchochea shughuli za kiuchumi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Barabara hii ya Makongoro ni fupi kuunganisha mikoa ya Tabora na Singida na mingineyo endapo itatupiwa jicho itakuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali na kuchochea miradi ya maendeleo ya kimkakati, ” amesema.