Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Juma Mwenda
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua rasmi mafunzo kwa wadau kuhusu Mfumo Jumuishi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS), mfumo mpya wa kodi za ndani unaotarajiwa kuanza kufanya kazi Februari 9 mwaka huu, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa walipakodi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo mapema Leo Januari 15 jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Juma Mwenda, alisema mfumo wa IDRAS utaondoa usumbufu wa walipakodi kufika ofisini mara kwa mara kwa kuwa huduma zitapatikana saa 24, popote walipo.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusufu Juma Mwenda
Alisema kupitia IDRAS, TRA itaweza kuwabaini na kuwabana wanaokwepa kodi, kusajili walipakodi wapya na wakati huohuo kulinda na kuwezesha biashara halali za walipakodi nchini.
Kamishna Mkuu huyo alibainisha kuwa mfumo huo utakuwa muarobaini wa utunzaji wa kumbukumbu za biashara kwa walipakodi, kwani taarifa zote zitahifadhiwa kwa usalama na kupatikana kwa urahisi.
Aidha, alisema IDRAS itatekeleza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuona mifumo ya taasisi za Serikali inasomana ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kupitia mfumo huo, walipakodi wataweza kutoa risiti za EFD bila kutumia mashine pamoja na kuomba na kupatiwa cheti cha kutokuwa na madeni ya kodi (Tax Clearance), hatua itakayorahisisha shughuli za kibiashara.
Kwa upande wake, Kamishna wa Kodi za Ndani, Alfred Mregi, alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa washauri wa kodi na wahasibu kwa siku tatu na kuendelea kwa makundi mengine kwa wiki mbili, ikiwa ni mkakati wa kuongeza uelewa wa jamii kabla ya mfumo kuanza rasmi.



