Umoja wa Mataifa wahoji uchaguzi mkuu kufanyika ‘gizani’ Uganda

Kampala. Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Ofisi ya Haki za Binadamu umehoji kuzimwa mitandao na kuitaka Uganda kuondoa marufuku kuzima intaneti, ikisema hatua hiyo inaiweka ‘gizani’ kwa kukosekana mawasiliano na uwazi wakati uchaguzi mkuu ukifanyika leo Alhamisi.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN imesisitiza kupitia ujumbe wa mitandao ya kijamii uliochapishwa Jumatano Januari 14, 2026 ikieleza kuwa upatikanaji wazi wa mawasiliano na taarifa ni muhimu kwa uchaguzi huru na wa kweli.

 “Waganda wote lazima waweze kushiriki katika kuunda mustakabali wao na mustakabali wa nchi yao.” ilieleza taarifa hiyo.

Utekelezaji wa agizo kukatwa intaneti ulianza Jumanne jioni baada ya Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) kuwaagiza waendeshaji wa mitandao ya simu kuzuia upatikanaji wa intaneti kwa umma.

Taasisi ya ufuatiliaji wa intaneti, NetBlocks, imesema hatua hiyo inaweza kupunguza uwazi na kuongeza hatari ya udanganyifu wa kura.

UN pia imetahadharisha kwamba huenda Waganda wakapiga kura katika mazingira ya ukandamizaji na vitisho dhidi ya upinzani wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wale wenye maoni ya kupinga.

Tume ya Mawasiliano ya Uganda imetetea hatua ya kuzima intaneti ikisema ni muhimu kudhibiti taarifa za upotoshaji, udanganyifu wa kubaini kuibuka vurugu zinazohusiana na uchaguzi mkuu.

Mkurugenzi wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki na Kusini, Tigere Chagutah ametaja hatua ya kuzimwa kwa intaneti kuwa ni shambulio la wazi dhidi ya haki ya uhuru wa kujieleza, akibainisha athari zake kubwa kwa uhuru wa kusafiri, maisha ya watu, na upatikanaji wa taarifa.

Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, anakabiliwa na upinzani kutoka kwa mwanasiasa, Robert  Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, huku kukiwa na wagombea wengine sita wanaowania nafasi hiyo.