Dar es Salaam. Pengo lililopo kati ya tafiti zinazofanywa katika taasisi za elimu ya juu na mahitaji halisi ya wafanyabiashara limeendelea kudaiwa kuwa kikwazo kikubwa, katika maendeleo ya biashara ndogo na za kati Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
Hali hiyo imebainika kuhitaji mabadiliko ya haraka ili tafiti za kitaaluma ziweze kutatua changamoto za wajasiriamali, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya teknolojia masoko na ushindani wa kimataifa.
Hayo yamesemwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi Bandari Tanzania (TPA), Dk Baraka Mdima, Januari 15, 2026, wakati wa ufunguzi wa kongamano la 20 la Afrika la Ujasiriamali na Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati (ICAESB), lililoandaliwa na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS). Dk Mdima amesema taasisi za elimu ya juu zinapaswa kuhakikisha tafiti zinazofanywa zinatumika moja kwa moja kuwasaidia wafanyabiashara na wajasiriamali.
Dk Mdima amesema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu kwa zaidi ya miaka 20, likiwakutanisha wasomi, watunga sera, wataalamu wa sekta binafsi na viongozi wa viwanda, huku likionesha wajibu wa shule za biashara kuhamisha maarifa kutoka vyuoni kwenda katika matumizi ya vitendo. Amebainisha kuwa biashara ndogo na za kati ndizo mhimili mkuu wa uchumi, hivyo mkutano huu unatoa nafasi ya kujadili mikakati ya kuendeleza biashara hizo ili ziweze kuendana na mabadiliko ya soko, teknolojia na biashara za kimataifa.
Mbali na changamoto za pengo la tafiti na mahitaji ya wafanyabiashara, kongamano hilo limeangazia umuhimu wa ubunifu, teknolojia ya kidijitali, uendelevu, ushiriki wa sekta binafsi na usimamizi wa kisasa. Dk Mdima amesema matokeo ya tafiti yanapaswa kutumika kuboresha sera, kuimarisha mifumo ya biashara, kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa Taifa.
Naye Profesa Omari Mbura, Mwenyekiti wa kongamano hilo, amesema mkutano huo unawawezesha wadau kujifunza changamoto zinazowakabili wajasiriamali, hususan biashara ndogo na za kati, na kutafuta njia za vitendo zitakazowawezesha kutumia maarifa yanayozalishwa vyuoni. Amesema changamoto kubwa ni tafiti nyingi kuandikwa kwa lugha ya kitaaluma, jambo linalofanya wafanyabiashara wengi kutoweza kunufaika, hivyo kuna haja ya uwasilishaji rahisi wa matokeo ili yafikie watumiaji wa kawaida.
Kwa upande wake, Pamela Kishimbo kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) amesema tafiti zake zinaonesha mitandao ya kijamii inaweza kuwa chombo chenye tija kwa wajasiriamali, hususan vijana na wanawake, ikiwa itatumika kwa malengo ya biashara na si burudani pekee. Mhadhiri wa UDBS, Benjamini Sakita, ameongeza kuwa tafiti zinapaswa kuendana na uhalisia wa jamii, zenye lugha rahisi na zenye kutoa suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi, vinginevyo faida itabaki kwa wachache tu wa ngazi ya kitaaluma.