Wananchi milioni 21.6 kupiga kura kumchagua Rais wa Uganda leo

Uganda. Wapigakura milioni 21.6  wanatarajiwa kupiga kura  katika uchaguzi mkuu wa kumchagua rais wa awamu ya saba wa  Uganda leo.
 Nchi hiyo inafanya uchaguzi mkuu leo Alhamisi Januari 15, 2026, huku kukiwa na mjadala kutokana na hatua ya serikali kuzima  intaneti jambo ambalo  upinzani unahoji mazingira ya kuwepo uchaguzi huru na  haki.

Mtandao wa TaifaLeo umeripoti kuwa, vituo vya upigaji kura vimefunguliwa saa 12 asubuhi na upigaji kura utahitimishwa saa 11 jioni. 
Vilevile wananchi wa Uganda katika uchaguzi huo pia watawachagua wabunge wapya.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda, Simon Byabakama amesema matokeo yanatarajiwa kutangazwa ndani ya saa 48 baada ya upigaji kura kumalizika. 
Hii ina maana mshindi  atatangazwa kabla ya Jumamosi saa 12 jioni.

Awali, Byabakama aliwaambia wanahabari kuwa, matokeo yatatangazwa kwa ngazi ya wilaya kisha yatumwe kwa kituo kikuu cha kujumuisha kura Lubowa, Wilaya ya Wakiso.

Ndani ya siku hizo mbili tume itatathmini na kujumuisha kura kabla ya mshindi wa urais kutangazwa.

Rais Yoweri Museveni ametangaza Januari 15 na Januari 16 kama siku za mapumziko ili kuwaruhusu Waganda kushiriki uchaguzi mkuu.

Washindani wawili kwenye uchaguzi huo ni  Museveni anayetetea nafasi yake ya urais baada ya kuongoza nchi hiyo tangu 1986 akigombea kupitia chama tawala cha NRM.

Mwanasiasa msanii Robert Kyangulanyi, maarufu Bobi Wine naye atakuwa akijaribu bahati yake kwa mara ya pili baada ya kupoteza kwa Museveni miaka mitano iliyopita (2021).

Wine amejizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana na anawania kupitia NUP. Katika uchaguzi wa 2021 alipata asilimia 35 ya kura zilizopigwa.

Hali ya usalama imeimarishwa maeneo mbalimbali ya nchi hiyo huku magari ya kijeshi na wanajeshi wenyewe wakiimarisha doria katika barabara mbalimbali.
 Tangu Uganda ipate uhuru wake mwaka 1962 haijawahi kuwa na mfumo wa kubadilishana madaraka.

Baadhi ya raia wametilia shaka uwazi kwenye kura hiyo wakisema hali hiyo inaendeleza utawala wa Museveni.

“Katika historia, hakuna uchaguzi ambao umewahi kuwa huru kwa sababu Museveni anatumia mabavu kupata ushindi,” amesema Opolot Jerome.

“Sasa hakuna intaneti na upigaji kura unatarajiwa kuendelea kwa kutumia mashine na teknolojia ya kisasa. Hiyo itawezekanaje?” amehoji Maria Teremwa.

“Kampeni zenyewe zimegubikwa na fujo, wafuasi wa upinzani wanapigwa. Sioni kama wengi watajitokeza kushiriki upigaji kura,” ameongeza Taremwa.

Alipokamilisha kampeni zake juzi Jumanne, Wine ambaye alikuwa amevalia helmeti ya kujikinga risasi, aliwataka vijana washiriki uchaguzi na kulinda kura zao.

Misafara ya kampeni za Wine (43), imekuwa ikiandamwa na fujo, akirushiwa mabomu ya machozi, wafuasi wake wakikamatwa na polisi kumwekea vizuizi barabarani.

Katika uchaguzi mkuu wa 2021, ghasia zilizuka ambapo zaidi ya watu 50 walikufa huku mamia ya wafuasi wa Wine wakikamatwa jijini Kampala.

Museveni katika kampeni zake amekuwa akijinadi kwa kuleta utulivu na Uganda huku akiahidi kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo.

Bobi Wine  amekuwa akiahidi mabadiliko, akisema utawala wa Museveni umechangia umaskini nchini humo.