Uganda. Wananchi wa Uganda wamejitokeza vituo vya kupiga kura katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo, huku baadhi maeneo ikiripotiwa ikichelewa kuanza shughuli ya kupiga kura hadi saa nne kamili asubuhi.
Vituo hivyo vya kupiga kura vimefunguliwa saa 1:00 asubuhi katika maeneo mbalimbali nchini humo katika uchaguzi mkuu unaofanyika leo Alhamisi Januari 15, 2026. Lakini baadhi ya maeneo ya Kampala na nje ya jiji hilo imeripotiwa wananchi kuchelewa kuanza upigaji kura.
Vituo kadhaa vya kupigia kura jijini Kampala na maeneo mengine ya nchi pia vimeripotiwa kuchelewa kuanza kwa shughuli ya upigaji kura, huku wasimamizi wa uchaguzi wakieleza sababu za zikiwamo za kimtandao.
Watu wanasubiri nyenzo za kupigia kura katika kituo cha kupigia kura mjini Kampala mnamo Januari 15, 2026. PICHA na ABUBAKER LUBOAA
Katika eneo la Makindye Ssabagabo, mgombea urais Conservative Party (CP), Joseph Mabirizi amelazimika kuondoka katika kituo cha kupigia kura bila kupiga kura baada ya maofisa uchaguzi kushindwa kuanza hatua hiyo hadi saa 4:00 asubuhi.
Mgombea huyo hakuweka bayana iwapo angerudi kabla ya vituo kufungwa jioni.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Daily Monitor wa Uganda unaoripoti hatua kwa hatua uchaguzi huo mubashara, katika kituo cha kupigia kura cha Lufuka Playground, Makindye Ssabagabo, vifaa vya kupigia kura havikuwa vimewasili hadi saa 4:00 asubuhi.
Afisa wa polisi na wanajeshi wanaonekana katika kituo cha kupigia kura mjini Kampala Januari 15, 2026, kabla ya uchaguzi wa kitaifa. PICHA/ABUBAKER LUBOWA
“Sishangazwi na ucheleweshaji huu kwa sababu serikali hulazimika kufanya hivyo Kampala kwa kuwa ni ngome ya upinzani,” amesema Mabirizi alipokuwa anaondoka kituoni.
Sehemu nyingine za Kampala imeripoti ucheleweshaji, yakiwemo baadhi ya maeneo ya Banda na Nakivubo, kituo kimoja cha kupigia kura katika Barabara ya Hannington karibu na makao makuu ya Benki ya Stanbic, pamoja na sehemu za Wilaya ya Biashara ya Kati.
Katika Najjera 1, eneo jingine ambalo ni ngome ya upinzani, upigaji kura haukuanza hadi saa 4:00 asubuhi katika vituo kadhaa, vikiwemo St Mark na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), ingawa katika vituo vingine kama Shule ya Msingi ya Quality na Namuwongo, upigaji kura ulikuwa umeanza, lakini kwa kuchelewa baada ya saa 3:00 asubuhi.
Katika maeneo mengine nchini Uganda imeripotiwa kuchelewa kuanza kupiga kura hususani katika Manispaa ya Kabale, Kusini-Magharibi mwa Uganda.
Katika Uwanja wa Kabale, wasimamizi wa vituo, Benson Musinguzi na Beth Nyakisa, wameieleza The Monitor kuwa upigaji kura haukuanza kutokana na hitilafu katika mfumo wa kupiga kura kwa njia ya bayometria, licha ya vifaa kuwasili kwa wakati.
Afisa wa Tume ya Uchaguzi akitayarisha vifaa vya kupigia kura wakati upigaji kura ukiendelea Kampala, Uganda Januari 15, 2026. PICHA na ABUBAKER LUBOWA
Matatizo kama hayo yaliripotiwa katika kituo cha Kabale, ambapo msimamizi Beth Nyakisa ametaja hitilafu za misimbo ya uthibitishaji kuwa chanzo cha ucheleweshaji.
Waganda wamejitokeza kupiga kura huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiwa vimeimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Rais Yoweri Museveni, aliye madarakani kwa karibu miongo minne, anatetea nafasi yake kwenye uchaguzi huo mkuu unaowajumuisha wagombea wengine wa urais kutoka vyama vya siasa saba.
Museveni, mwenye umri wa miaka 81, ameongoza nchi hiyo tangu mwaka 1986, anawania muhula mwingine wa miaka mitano dhidi ya wagombea saba, wakiongozwa na kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.
Juzi, Jumanne Serikali ya Uganda iliagiza kufungwa huduma ya intaneti kwa umma na kuzuia baadhi ya huduma za simu, hatua ambayo imesema inalenga kuzuia upotoshaji wa taarifa na machafuko.
Makundi ya kutetea haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani wamesema hatua hiyo imepunguza nafasi ya ushiriki wa kiraia na kudhoofisha uwazi.
Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) iliamuru kampuni za mawasiliano kukata huduma ya intaneti nchini kote hadi hapo itakapotolewa amri ya kuondoa zuio hilo.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya misukosuko wakati wa kampeni ambapo iliripotiwa kukamatwa wafuasi wa upinzani, pamoja na matumizi ya risasi za moto na gesi ya kutoa machozi mara kwa mara katika mikutano ya kampeni inayohusishwa na Bobi Wine.
Wagombea wanane wanaochuana katika uchaguzi huo wa urais wa Uganda ni Rais anayetetea nafasi yake Yoweri Museveni wa Chama cha National Resistance Movement (NRM), kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi (Bobi Wine) wa National Unity Platform (NUP), Mugisha Oyera wa Alliance for National Transformation (ANT).
Rais Museveni akipiga kura katika kituo cha kupigia kura cha Shule ya Upili ya Karo huko Rwakitura Januari 15, 2026. PICHA/SCREEN-GRAB/UBC
Wengine ni Nathan Mafabi wa Forum for Democratic Change (FDC), Joseph Elton Mabirizi wa Conservative Party (CP), Robert Kasibante wa National Peasants Party, Mubarak Munyagwa Sserunga wa Common Man’s Party (CMP), na Frank Bulira Kabinga wa Revolutionary People’s Party (RPP).
