Winga Msenegali bado kidogo Simba, wengine watatu wakitajwa

MABOSI wa Simba wapo katika hatua ya mwisho ya mazungumzo kabla ya kushusha winga mpya kutoka Senegal, lakini kukiwa na taarifa kuna mashine nyingine tatu zikiwa katika mazungumzo ya kutua Msimbazi, huku baadhi ya mastaa waliopo kikosini wakiwa mbioni kuondolewa.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba mabosi wa kikosi hicho kwa sasa wako bize sokoni kwa ajili ya kufanya maboresho makubwa kabla ya dirisha la usajili halijafungwa Januari 30, 2026 kwa lengo la kumrahisishia kocha mkuu mpya, Steve Barker.

Simba inayosota kusaka mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kuyakosa kwa misimu minne mfululizo, inadaiwa ipo katika hatua nzuri kumbeba winga Libasse Gueye kutoka FC Teungueth, lakini ikipiga hesabu pia kuwatoa kwa mkopo nyota watatu waliopo sasa.

Nyota wanaopigiwa hesabu kutolewa Msimbazi ni winga Joshua Mutale, straika Steven Mukwala na beki wa kati Chamou Karaboue ili kuruhusu mashine nyingine mpya zitue na kumrahisishia kazi Barker aliyetua kikosini hivi karibuni kutoka Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli inapambana kutafuta timu za kuwapeleka kwa mkopo nyota wa kigeni zaidi ya watatu ili kupisha usajili mwingine bora kwa matakwa ya benchi la ufundi, ikielezwa kuna majina manne mezani.

Nyota wa kwanza ni beki wa kati Mkongomani Ndongani Samba Gilbani anayeichezea Asante Kotoko yenye makao makuu Kumasi katika Mkoa wa Ashanti Ghana, aliyojiunga nayo Julai 11, 2024, baada ya kuachana na kikosi cha Rahimo cha Burkina Faso.

Taarifa zinaeleza uongozi wa Simba hauridhishwi na mwenendo wa beki wa kati wa kikosi hicho, Chamou aliyejiunga na timu hiyo Agosti 7, 2024, akitokea Racing Club Abidjan ya kwao Ivory Coast, jambo linaloufanya kuingia sokoni.

MSENE 01

Ndongani anayehusishwa pia na Azam inayodaiwa iliweka kiasi kikubwa cha fedha ili kumsajili, inaelezwa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam wamelegeza kamba kwa beki huyo, ambapo kwa sasa wametoa nafasi zaidi kwa Simba kuiwania saini yake.

Mbali na Ndongani, nyota mwingine aliyepo katika mazungumzo na Simba ni kiungo mkabaji Genino Tyrell Palace ambaye kwa sasa anacheza Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, ikiwa ni pendekezo la Kocha Barker aliyewahi kufanya naye kazi.

Genino aliyezaliwa Desemba 19, 1998, huko Afrika Kusini ana uzoefu mkubwa baada ya kuzichezea pia, timu za vijana chini ya miaka 19 ya SG Sacavenense, Braga (U-23) na Academica (U-23) zote za Ureno, kisha kurejea nyumbani Maritzburg United.

Kiungo huyo anayesifika kwa uwezo mkubwa wa kukaba, alijiunga na Stellenbosch Julai 25, 2023, akitokea Maritzburg United zote za Afrika Kusini, ambapo kwa sasa Barker amempendekeza asajiliwe ili akaungane naye tena akiwa Simba.

Beki wa kushoto raia wa Mauritania, Khadim Diaw aliyekuwa akihusishwa tangu dirisha kubwa la usajili lililopita, pia ni nyota mwingine anayekaribia kujiunga na timu hiyo baada ya kudaiwa mazungumzo kwa sasa yapo katika hatua nzuri zaidi.

Diaw aliyezaliwa Juni 7, 1998, alikuwa akihitajiwa na Simba tangu alipokuwa Kocha Fadlu Davids, ambapo kwa sasa mabosi wa kikosi hicho wanafanya mazungumzo ya kumsajili baada ya nyota huyo kuachana na Al Hilal Omdurman ya Sudan.

Mabosi wa Simba wanaamini wanaweza kumpata beki huyo kwa urahisi kwa sababu yupo huru, ambapo amewahi kuzicheza timu za Generation Foot ya Senegal na Horoya AC ya Guinea, kisha kuondoka rasmi Juni 26, 2023 na kujiunga na Al Hilal Omdurman.

Nyota mwingine pia anayewindwa na Simba ni kiungo mshambuliaji Gueye anayeichezea Teungueth FC ya kwao Senegal. Mchezaji huyo pia amekuwa akihusishwa na mabwenyenye wa Algeria, USM Alger.

Gueye ni miongoni mwa nyota wanaovutia timu nyingi kutokana na uwezo wake wa kushambulia akitokea katikati na upande wa kulia pamoja na kushoto, huku akicheza pia Demba Diop kuanzia vijana hadi ya wakubwa na Diambars FC zote za kwao Senegal.

MSENE 02

Pia, ameitumikia timu ya vijana chini ya miaka 19 ya Valencia na Pontevedra CF inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu zote za Hispania, ambapo mchezaji huyo mwenye miaka 22, anatajwa ni kuwa miongoni mwa viungo bora anayetabiriwa kufika mbali zaidi.

“Timu tayari imefanya usajili wa wachezaji wanne wa kigeni hadi sasa kwa nafasi tofauti kama benchi la ufundi lilivyotaka. Kuhusiana na winga unayemzungumzia makubaliano baina ya mchezaji na klabu tumekamilisha,” kilisema chanzo na kuongeza:

“Kilichobaki ni mazungumzo na klabu yake ambayo pia hatuoni kama itaweka ugumu kutokana na kufikia ofa waliyoitaka ili kumuachia mchezaji huyo. Mambo yakienda vizuri kila kitu kitawekwa wazi.”

Chanzo hicho kilisema usajili wanaofanya sasa ni mapendekezo ya benchi la ufundi ambalo ndio limeona upungufu katika nafasi hizo tulizosajili na naamini utakuwa chachu ya kuitoa timu yao nafasi walitopo.

“Hatupo vizuri tangu misimu minne iliyopita tukikosa mataji, hatutaki kupoteza tena msimu huu licha ya kutokuwa na matokeo mazuri, lakini tumeshindwa kufikia malengo kimataifa. Hii haikubaliki tunatakiwa kuirudisha timu kwenye ubora na ushindani,” chanzo hicho kilisema.

“Usajili unaofanyika sio tu wa kujaza nafasi tunawaahidi mashabiki kuwa utaleta taswira nzuri shindani ndani na kimataifa, lengo siyo tu kufikia malengo lakini pia ni kuirudisha timu pamoja na mashabiki ambao wamekata tamaa.”

Chanzo hicho kiliongeza kwamba hadi sasa viongozi wamekamilisha usajili ambao walipanga kuufanya katika dirisha hili na muda wowote kuanzia sasa wataanza kutambulisha wachezaji wapya ambao wataongeza chachu ya ushindani kikosini.

Kutokana na kanuni inayotaka klabu kuwa na wachezaji 12, mabosi wa Simba wanafanya mpango kuwatoa mastaa hao watatu kwa mkopo kutokana na kuwa na mikataba nao, huku ikielezwa Mukwala kuna dili la kutaka kununuliwa jumla linasikiliziwa.

Mutale na Karaboue walikuwa na kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 iliyomalizika juzi Zanzibar, Wekundu hao walitolewa nusu fainali na Azam FC iliyopoteza mechi ya fainali mbele ya Yanga iliyobeba taji la pili msimu huu baada ya Ngao ya Jamii.